23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 5, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yawafunda wafanyabiashara kutunza kumbukumbu

KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

BIASHARA yoyote ili iweze kufanikiwa hadi kuwa kubwa, ni lazima mfanyabiashara awe na utaratibu wa kutunza kumbukumbu.

Biashara isiyotunziwa kumbukumbu uwezekano wa kupatikana kwa hasara bila mhusika kujua ni mkubwa kuliko yule anayetunza.

Kuna msemo unaosemwa kuwa mali bila daftari hupotea bila habari, ambao hutumika kuwakumbusha au kuwahamasisha wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zao ili kuepusha hasara zisizo za msingi.

Hivi majuzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) kwaajili ya kuwapa mbinu za namna ya kuweza kufanikiwa katika biashara zao ikiwa ni pamoja na nchi kupata maendeleo kutokana na kodi watakazolipa.

Katika mkutano ule, wafanyabiashara walifundishwa masuala ya kodi pamoja na namna ya kutunza kumbukumbu za biashara zao ili kuepuka kupata hasara, lakini pia kuweza kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya mkutano wao na JWT, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Msafiri Mbibo, anasema mkutano huo ulilenga kubadilishana uzoefu, kuangalia changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kodi kutokana na mabadiliko ya sheria ambayo hujitokeza mara kwa mara.

Anasema kumekuwapo changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, na kwamba kwa upande wa wafanyabiashara baadhi ya changamoto hizo hutokana na kutokuwapo kwa utunzaji wa kumbukumbu za biashara.

“Mali bila daftari hupotea bila habari hivyo, ili kuweza kufanikiwa na kufikia malengo kila mfanyabiashara anatakiwa kutunza kumbukumbu za biashara zake ili kudhibiti mwenendo wa shughuli anazofanya hatimaye kuepuka hasara zisizo za msingi,” anasema Mbibo.

Anasema kwa mujibu wa sheria, kila mwenye mapato anatakiwa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi hivyo, wananchi wanatakiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Anaongeza kuwa bila huduma ya umeme, maji, barabara, ulinzi na usalama pamoja na miundombinu, biashara haziwezi kufanyika hivyo, TRA na wafanyabiashara ndio wanaoweza kufanikisha hayo kwa kuwa wazalendo katika suala zima la ulipaji na ukusanyaji wa kodi.

Anasema katika kuhakikisha TRA inafanikisha kukusanya mapato hadi kufikia lengo, mamlaka hiyo imejipanga kuwafikia wafanyabiashara nchi nzima ili kuwapa elimu ya kodi, kutanua wigo wa kodi ikiwa ni pamoja na kuongeza walipakodi wapya.

“Kitu kingine kinachotakiwa ni wafanyabiashara kuungana katika makundi ili kuweza kuzungumza lugha moja na serikali itakayoiwezesha kuimarisha miundombinu na mifumo mingine itakayowezesha maendeleo,” anasema Mbibo.

Anasema ili kufikia malengo waliyojiwekea katika suala la utoaji elimu na ukusanyaji wa mapato ya serikali, TRA itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara ili waweze kulipa kodi kwa hiyari.

Sambamba na hilo, anasema mamlaka hiyo itaendelea kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake yatakayowawezesha kukokotoa kodi kwa weledi bila kumuonea mtu, lakini pia kodi ya serikali ipatikane kihalali na kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kuiwezesha TRA na wafanyabiashara kuwasiliana vizuri.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Mchungaji Silver Kihondo, anasema mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu za biashara yataleta manufaa ikiwa ni pamoja na kupunguza malalamiko yasiyo na tija.

Anasema sambamba na mafunzo hayo, watawasilisha changamoto ambayo bado haijafanyiwa kazi, wafanyabiashara kukutana na gharama za uendeshaji zisizo na stakabadhi ambazo hazitambuliki kisheria.

Anasema serikali inatakiwa kuzitambua changamoto hizo na kuziweka katika sheria ili kuwasaidia kupunguza mzigo.

“Tunashukuru kwa mafunzo mazuri ya utunzaji kumbukumbu ambayo naamini yataleta uponyaji kwa wafanyabiashara, lakini ombi letu kubwa kwa TRA ni kutambua gharama za uendeshaji biashara tunazokutana nazo ambazo hazina stakabadhi. Pia jambo hili tungependa litambuliwe kisheria ili kuepuka kuwa mzigo kwa wafanyabiashara,” anasema Mchungaji Silver.

Naye Jackline Francis, ambaye ni mfanyabiashara wa duka la vyombo maeneo ya Kimara, anasema elimu ya utunzaji wa kumbukumbu itawasaidia kutokana na kuwa baadhi yao wamekuwa wakifanya biashara kwa mazoea badala ya kufuata taratibu za biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles