Na Paul Kayanda, Kahama
MMOJA wa wachimbaji wadogo machimbo ya Nyangarata, waliookolerwa baada ya kufukiwa na kifusi mgodini kwa siku 41, Onyiwa Kaiwao (55) amefariki dunia.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi, alisema kuwa Kaiwao alifariki dunia jana saa 6.00 mchana baada ya kupata matatizo na kushindwa kupumua.
“Ni kweli amekufa na sababu ya kifo chake inaonekana wakati akitapika na huku akiwa amelala.
“Sehemu ya matapishi yake yaliingia kwenye njia ya hewa na hivyo kusababisha mauti kumfika,” alisema.
Dk. Ngowi alisema mgonjwa huyo aliugua numonia, ugonjwa unaosababishwa na baridi kali iliyowakumba wachimbaji hao wakiwa shimoni na hali yake ilibadilika ghafla.
Alisema sababu nyingine ni tatizo ambalo lilianza kujitokeza siku za hivi karibuni la kujisaidia vipande vya magome ya miti ambayo walikuwa wakila shimoni kama chakula.
“Jana (juzi) tuliwachukua vipimo wote watano na kuonyesha kuwa hali zao ni nzuri lakini huyo alionyesha kutokuwa na maendeleo mazuri tofauti na wenzake.
“Ghafla akiwa amelala alianza kutapika na leo (jana) alifariki dunia,” alisema Dk. Ngowi.
Alisema wachimbaji wengine hali zao zinaendelea vema na kwamba iwapo kutajitokeza lolote basi itaangaliwa uwezekano wa kuwahamishia Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
“Sasa tutakuwa tukiwapima kila mara kuangalia afya zao lakini tukiona dalili za mabadiliko ya afya yao haraka sana tutawahamishia Bugando kwa matibabu zaidi,” alisema.
Wachimbaji hao watano waliokolewa mwanzoni mwa mwezi huu baada kukaa chini mgodini huo kwa siku 41.
Wakiwa shimoni walikuwa wakila nguo, magome ya miti na udongo na kukinga maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka juu ardhini kwa kutumia kofia ngumu (helmet).
Mmoja wao alifariki dunia wiki chache baada ya kufukiwa kwa ugonjwa wa kuharisha.