26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Samia aeleza muhimu utunzaji vyanzo vya maji

Ramadhan Hassan -Dodoma

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa ujenzi bwawa la kufua umeme maporomoko ya Mto Rufiji, mikakati iwekwe kuhakikisha vyanzo vya maji katika mto huo havikauki.

Agizo hilo amelitoa jana jijini hapa, akifungua jukwaa la sita la maendeleo endelevu kuhusu usimamizi madhubuti wa misitu kwa upatikanaji rasimali maji endelevu.

Samia alisema Serikali ikipeleka fedha nyingi katika mradi wa kufufua umeme Mto Rufiji, wana jukumu kubwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kutiririsha maji bila kuzuiwa.

“Wakati tunatumbukiza fedha nyingi kwenye mradi wa kuzalisha umeme Mto Rufiji, tufahamu tuna jukumu kubwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kutiririsha maji bila kuzuiwa na shughuli yoyote,” alisema.

Alisema mradi huo utategemea mtiririko endelevu wa maji kutoka vyanzo vikuu,  ikiwamo mito na madakio ambayo yanaanzia kwenye misitu.

Samia alisema kilimo kisichokuwa endelevu, ujenzi holela, uchomaji mkaa, ukataji kuni, uvunaji haramu wa magogo na ufugaji usiozingatia kanuni, vimekuwa vikisababisha athari kwa uhai wa rasilimali hizo.

“Mto Ruaha Mkuu ambao ni tegemeo kubwa kwa ustawi wa wanyamapori na uzalishaji umeme kwenye mabwawa ya Mtera na Kidau, umeathiriwa na shughuli za kibinadamu, ndiyo maana uzalishaji nishati umekuwa wa kusuasua,” alisema.

Kutokana na hali hiyo Samia aliziagiza taasisi na mamlaka husika kushirikiana na wadau kuongeza jitihada ya kusimamia ipasavyo rasilimali hizo.

Hata hivyo, alisema zipo jitihada za Serikali kuboresha utunzaji na utumiaji rasilimali misitu na maji ambazo zimeanza kuonyesha mafanikio katika baadhi ya maeneo.

“Mamlaka za mabonde ya maji zimeimarisha uwajibikaji katika matumizi endelevu ya maji. Takwimu zinaonyesha ongezeko la upatikanaji maji vijijini kutoka asilimia 40 na 50 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita,” alisema.

Aidha, alisema Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48 ambazo zinasimamiwa kupitia taratibu mbalimbali.

Samia alisema takwimu zinaonyesha kiasi cha upotevu wa misitu kwa sasa ni kikubwa hivyo pasipo jitihada tunaweza kujikuta misitu haipo tena.

“Mathalani, kasi ya kutoweka misitu na uoto wa asili inasadikiwa kuwa kubwa. Takwimu za mwaka 2015 zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, zinaonyesha kwamba Tanzania inapoteza hekta 372,816 kwa mwaka,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, alisema jukwaa hilo linajadili namna ya kusimamia rasilimali misitu na maji kuleta uendelevu wa rasilimali hizo muhimu.

Pia alisema wanajadili sera na mifumo ya kitaasisi, mahitaji ya rasilimali na mifano bora ya kiusimamizi.

“Sekta ya misitu na maji zinategemeana na kuimarishana pale zinapotunzwa. Ni vyema sera, mikakati na taasisi zinazozihusu zikafungamana ili zifanye kazi kwa ufanisi,” alisema Profesa Semboja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles