Christina Gauluhanga-Dar es salaam
WAAJIRI nchini wametakiwa kutoa kipaumbele kwa wanawake katika nafasi za uongozi kwakuwa wengi wao wameonyesha mafanikio katika nyadhifa mbalimbali walizonazo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu uzinduzi wa mkutano mkuu wa pili wa wanawake katika uongozi kwa mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, alisema kwa mwaka huu watahakikisha kuwa wanazionyesha kampuni na taasisi mbalimbali njia bora za utekelezaji wa kanuni za Umoja wa Mataifa za kuwawezesha wanawake.
Alisema tafiti zinaonyesha kwa kufanya uwezeshaji, kampuni huongeza ufanisi sehemu za kazi na kusababisha kuongezeka kwa uzalishaji.
“Mkutano huu utafanyika Septemba 19, mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo umebeba kaulimbiu isemayo ‘Mustakabali wa ajira za wanawake kwa wakati ujao. Je, sera za mahali pa kazi zipo tayari’, lengo likiwa ni kuwaleta viongozi wa kampuni, mashirika binafsi na umma, taasisi na wadau wa uongozi ili kujadiliana uwepo wa sera zinazochochea kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi,” alisema Dk. Mlimuka.
Alisema kwa mwaka huu mkutano huo mkuu wa pili umeandaliwa na ATE kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri nchini Norway (NHO), pamoja na UN Global Compact Network Tanzania (UNGCN), ambapo pia utaambatana na mahafali ya tatu ya programu ya mwanamke wakati ujao.
Alisema malengo ya mkutano huo ni kujadiliana changamoto zinazowakabili viongozi wanawake na fursa zinazohusiana na mustakabali wa ajira za wanawake wakati ujao.
Pia kubadilishana ujuzi, kuzindua rasmi utekelezaji wa kanuni za Umoja wa Mataifa za uwezeshaji wanawake na kusherehekea mafanikio ya programu ya mwanamke tangu ilipoanzishwa mwaka 2016.
Kwa upande wake, Mratibu wa UN Global Compact Network Tanzania, Emmanuel Nnko, alisema wakati sasa umefika kwa waajiri kuendelea kutoa kipaumbele kwa nafasi za uongozi kwani wengi wameonyesha wana uwezo wa uzalishaji.
Alisema ni wakati sasa kwa kampuni kutoa fursa kuonyesha usawa wa kijinsia, mahusiano kazini na kufanya biashara endelevu hasa wakati huu wa kuelekea uchumi wa viwanda.