ELIZABETH HOMBO Na LEONARD MANG’OHA
WADAU mbalimbali na wananchi wametoa maoni yao kuhusu bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/20 itakayosomwa leo bungeni Dodoma, huku wengi wao wakishauri iguse maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, alisema wana imani kuwa bajeti hiyo itagusa masilahi ya walimu kuanzia madeni yao ya muda mrefu.
“Pia tunatarajia kuona madaraja yanapandishwa kwa walimu, kwa mfano changamoto iliyopo hivi sasa idadi ya wanaopandishwa madaraja ni ndogo kuliko inavyotakiwa, hivyo Serikali iangalie hili.
“Kingine ni upungufu wa walimu, hasa shule za msingi. Pamoja na kwamba Serikali imetoa ajira nyingi, lakini bado ni wachache, hivyo tunaomba angalau kila mwaka Serikali itoe ajira 10,000 kwa walimu,” alisema Seif.
Mchumi kutoka Taasisi ya Utafiti ya Repoa, Dk. Lucas Katera, alisema matarajio yake ni kwamba bajeti hiyo itajikita kwenye kuwekeza masuala ya viwanda.
“Ukizingatia Serikali ya awamu ya tano imekuja na uchumi wa viwanda, hivyo ni wazi kwamba hata bajeti hii ya 2019/20 itaangalia masuala ya kuwekeza viwanda ikiwa ni pamoja na miundombinu na huduma za jamii,” alisema Dk. Katera.
Profesa Haji Semboja wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema anapotazama vipaumbele vya mpango wa maendeleo, ni yale mambo mazuri yaliyoahidiwa na Serikali wakati wa Uchaguzi Mkuu na kwamba sasa wanatekeleza.
“Unapowekeza fedha nyingi kwenye miundombinu kwa ajili ya uchumi wa viwanda, lazima kuna sehemu zingine zinazorota, sasa hili linawafanya wananchi wajitegemee na wachangie kwenye maendeleo.
“Serikali ikitaka kukubeba lazima na wewe ujibebe na ndio maana Serikali inakusanya kodi. Pia wananchi lazima wanatakiwa wawekeze kwenye kilimo cha kisasa.
“Pia wajipange kujiweka katika kampuni zinazokopesheka na kukubalika. Hivyo matarajio yangu kwa ujumla ni mabadiliko ya akili ya kibinadamu kwamba Serikali imejenga reli je, impandishe mwananchi kwenye ndege? Si lazima atatoa nauli ndipo apande reli?
“Na kwenye ndege hivyo hivyo, kwamba Serikali imeleta ndege, sasa kazi ni kwamba mwananchi kupanda na si kupandishwa kwenye ndege na Serikali,” alisema Profesa Semboja.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara wadogo katika soko jipya la Mwege, Dar es Salaam, walisema wanatamani kuona bajeti ya mwaka mpya wa fedha ikigusa zaidi maisha ya wajasiriamali wadogo.
Michael Mmbwambo, alisema anatamani kuona bajeti itakayoangalia watu wa chini, wakiwamo wajasiriamali kwa kupunguza baadhi ya kodi kwa wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza bidhaa kutoka nje.
“Wafanyabiashara wakubwa wanalia na tozo nyingi wanapoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi, hali hii inawafanya wengi kuuza bidhaa hizo kwa bei kubwa na wengine kuingiza bidhaa ambazo si nzuri.
“Kwa mfano hapa nauza mitumba, unapopata mzigo mbaya hauuziki. Serikali ikiliangalia hilo mizigo itakuja mizuri,” alisema Mmbwambo.
Barnabas Shirima alisema bajeti ya mwaka ujao inapaswa kuangalia zaidi masuala ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo kwa kupunguza riba ili waweze kukopa na kuendesha biashara kwa sababu fursa zipo, lakini hawana mitaji.
Mbowe Yusuf alisema lazima bajeti ya mwaka huu iwekeze katika kutafiti hali ya uchumi ili kufahamu maeneo ya kipaumbele kutokana na hali ngumu inayowakabili wananchi wa kipato cha chini.
“Kwa miaka mitatu tumeona kipaumbele cha Serikali ni ujenzi wa miundombinu, hilo ni jambo zuri kwa sababu maendeleo huletwa na miundombinu, ila bajeti hii wawekeze kwenye utafiti wa hali ya uchumi,” alisema Yusuf.