26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri atangaza kufuta makanisa

Mathias Chikawe
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe

Na Gloria Tesha

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema atayafuta makanisa yote nchini ambayo yamekuwa yakitawaliwa na vurugu mara kwa mara.

Amesema pamoja na makanisa hayo kusajiliwa kwa ajili ya kumtumikia Mwenyezi Mungu, baadhi yamekuwa yakimtia aibu Mwenyezi Mungu, wanayemtumikia.

Chikawe aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza wakati wa maombi ya kuliombea taifa yaliyoandaliwa na Chama cha Kitume cha Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Maombi hayo yalifanyika katika Viwanja vya Kituo cha Maombi na Maombezi cha Emaus, kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.

“Siku hizi makanisa yanafanya mambo ya aibu sana, yaani viongozi wa makanisa wanapigana hadharani wakati wa ibada na wakati mwingine kufikishana polisi.

“Kwa mfano, hili Kanisa la Moravian, Jimbo la Misheni Mashariki ambalo kwa zaidi ya miaka miwili limekuwa na vurugu zinazohusisha shirika zake.

“Serikali haitavumilia vurugu makanisani, lazima tutachukua hatua na ikibidi mimi mwenyewe nitayafutia usajili makanisa yote yenye migogoro.

“Viongozi wa dini mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuchochea amani lakini sasa nyinyi ndiyo mnaoongoza kuchochea vurugu, hatuwezi kukubali, lazima tuchukue hatua,” alisema Chikawe.

Katika maombi hayo Chikawe aliwakilisha viongozi wa Serikali na viongozi wa kisiasa katika maombi hayo.

Kwa mujibu wa Chikawe, migogoro iliyoko makanisani imezidi kuongezeka kwa kuwa baadhi ya viongozi ni wabinafsi na ni wabadhilifu wa mali za makanisa yao.

“Waumini wanapigana wakati wa ibada, tujiulize ni mfano gani tunawaonyesha Watanzania wasio na dini.

“Kwa utaratibu huo, nani atatamani kuwa mkristo, katika hili, natumia fursa hii kuwakumbusha viongozi kuwa mfano wa kuigwa, ni lazima viongozi tuwe na hofu ya Mungu na tutumie nafasi zetu kujenga umoja, amani na mshikamano badala ya kuwa chanzo cha vurugu,” alisema Chikawe.

Aliwataka viongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania kumaliza mgogoro wao kwa busara na kutumia vitabu vya Mungu badala ya kushitakiana katika vituo vya polisi.

Katika maelezo yake, aliwataka wakasome kkatika Biblia Takatifu, Kitabu cha Waebrania 12:14.

Pamoja na hayo, alisema Tanzania haina dini lakini watu wake lazima wawe na tabia nzuri zinazowatofautisha na wengine.

“Nawaambia tena, kamwe Serikali haitavionea aibu vikundi wala makanisa yanayochochea vurugu na kama hayatabadilika na kutekeleza yale yanayopaswa kwa mujibu wa usajili, yatafutwa mara moja,” alisisitiza.

Akizungumzia suala la Katiba mpya, aliwataka Watanzania kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.

“Nawaombeni sana, tuombee mchakato wa Katiba mpya ili ufanikiwe kwa amani wakati wote na nayasema haya kwa sababu mnajua kinachoendelea kwa sasa,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Karismatiki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Merdad Banzi, alisema kilichosemwa na Waziri Chikawe lazima kifanyiwe kazi kwa kuwa ukweli unabaki kuwa Mungu ni Mfalme wa amani na hapendezwi na vurugu.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kwa kweli serikali isimame kidete kukomboa vurugu hizi. maana mimi binafsi sipendezwi na migogoro ya kidini hasa kwa kanisa la moravian. hii ni kwamba viongozi wa kanisa wnatawaliwa na tamaa na hatimaye kujikuta kufanya maamuzi nje na katiba yao isemavyo na kwa upande wangu viongo wenye nyazifa na wanaokubalika kuliongoza kanisa la mungu lazima wawe waadilifu na si sehemu ya mgogoro. hii imeendelea kuonekana ktk kanisa la moraviani kwa matumizi mabaya ya kuliendesha kanisa na hii inaonekana hasa kwa ngazi za majimbo yaani wenyeviti ndio chanzo cha migogoro yote. kitu pekee kiongozi inafaa awe mtu mwenye kupendwa na wengi na mwenye kutetea na kulinda kanisa siyo wa kulazimisha kuwa na madaraka bila kukubaliwa na waumini wote wa kanisa husika huku kulazimisha madaraka ndicho kitu pekee kinacho yafikisha makanisa hapa hasa kwa kanisa la moraviani jimbo la misheni mashariki. inaskitisha kuwa viongozi wa majimbo kuwa ndio sehemu ya mgogoro. Naiomba serikali iwachuguze kwa makani hawa viongozi kwa makini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles