NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka Afrika(Caf)limethibitisha Tanzania kuwalikishwa na timu nne katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu wa 2019-20.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF)jana,kupitia kwa ofisa habari wake , Cliford Ndimbo, timu mbili zitashiriki Ligi ya Mabingwa na nyingine mbili zitashiriki Kombe la Shirikisho.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, zilizofanyiwa marekebisho, Kamati ya Utendaji ya TFF, baada ya kupatikana nafasi nne, timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo ni Simba, Yanga, ambazo zitashiriki Ligi ya Mabingwa, wakati KMC na Azam FC zitashiriki Kombe la Shirikisho.
KMC itaiwakilisha Tanzania Kombe la Shirikisho, kwa mujibu wa kanuni hiyo ambayo inatamka, kama timu iliyomaliza nafasi ta tatu itakuwa ndio bingwa wa Kombe la TFF, basi mshindi wanne atapata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, bingwa wa Kombe la TFF atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Ikumbukwe kuwa , KMC ilimaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyomalizika wiki iliyopita, wakati Simba ilikata tiketi ya Ligi ya Mabingwa, baada ya kufanikiwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa ya Ndimbo iliendelea kufafanua kuwa, tayari caf imefungua dirisha kwa mashirikisho kusajili timu kupitia mtandao wa CMS huku mwisho wa kufanya hivyo ukitajwa kuwa Juni 30 mwaka huu, ambapo TFF inatakiwa iwe imesajili timu zitakazoshiriki kwenye mashindano ya kimataifa msimu wa 2019-2020.
Ilieleza kuwa, Rais wa TFF, Wallace Karia amezitaka klabu zilizopata nafasi kusajili kwa umakini na kujiandaa kwa mashindano ya Caf, ili kutopoteza nafasi ya kuingia timu nne katika mashindano hayo.
Makamu Mwenyeki wa Yanga, Fredrick Mwakaleba alipoulizwa namna walivyopokea taarifa hivyo ya Caf alisema;Kiukweli tumelipokea kwa furaha kubwa,na uzuri tunarudi kimataifa tukiwa na kikosi kipana na cha kupambana,ni imani yetu tutafanya vizuri”
Tanzania imepata nafasi hiyo, baada ya kuwa katika nafasi ya 12, kwenye viwango vya ubora vya Caf, hatua iliyochangiwa na mafanikio ya timu ya Simba katika ushiriki wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Simba ilifanikiwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutupwa nje ya mashindano hayo makubwa kabisa kwa ngazi ya klabu na timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) ililazimishwa suluhu Uwanja wa Taifa kabla ya kuchapwa mabao 5-1 katika mchezo wa marudiano jijini Lubumbashi.
Taarifa hiyo ya Caf ni wazi itapokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga ambayo awali ilipoteza kwa mara nyingine sifa ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa, baada ya kukosa fursa hiyo pia msimu wa 2018-2019.