25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bodi ya Mikopo yapanua wigo wanaotaka mikopo elimu ya juu

Na Mwandishi wetu

-Dar es Salaam

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imepanua wigo kwa wanaotaka mikopo ya elimu ya juu kwa kuongeza umri wa waombaji kutoka miaka 33 hadi 35 na kuongeza miaka kwa waliohitimu kidato cha sita na stashahada miaka ya nyuma kutoka miaka mitatu hadi mitano.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema sifa hizo zitaanza kutumika kwa waombaji wa mwaka wa masomo 2019/20.

“Baada ya kupokea maoni ya wadau, tumeongeza umri wa waombaji mikopo kutoka miaka 33 hadi 35 na pia mwaka huu tutapokea maombi kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita au stashahada ndani ya miaka mitano iliyopita… kabla ilikuwa miaka mitatu tu,” alisema Badru.

Aliongeza kuwa katika mwaka mpya ujao wa masomo, Serikali kupitia bodi hiyo imepanga kutoa mikopo na ruzuku ya elimu ya juu yenye thamani ya Sh bilioni 450 kwa wanafunzi 128,285, wakiwamo 45,000 wa mwaka kwanza, ikilinganishwa na Sh bilioni 427.5 zilitolewa kwa wanafunzi 123,000 mwaka huu wa masomo.

Alisema mfumo wa maombi kwa njia ya mtandao utafunguliwa Juni 15, na kufungwa Agosti 15 huku akiwataka kuusoma kwa makini na kuuzingatia maelekezo.

“Uzoefu wetu unaonesha kuwa waombaji wengi hukimbilia kwenye mtandao na kujaza fomu za maombi wakati mwingine bila kusoma mwongozo.

Mwaka huu tumetoa mwongozo huu kwanza ili wausome kwa wiki takribani mbili kabla ya kuruhusiwa kuanza kujaza fomu kwa njia ya mtandao,” alisema Badru.

Alisema katika mwaka 2018/2019, zaidi ya waombaji 9,000 kati ya 57,539 waliokuwa na sifa za msingi walikosea kujaza fomu za maombi.

Aliongeza kuwa ili kutatua changamoto hiyo kwa waombaji wapya, katika mwaka huu wa masomo bodi hiyo imetembelea shule 81 za sekondari katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar na kukutana na wanafunzi 27,489 ambao walielimishwa kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi.

“Pamoja na mwongozo huo, pia tumeandaa kijitabu chenye maswali na majibu yanayoelekeza namna ya kuomba mkopo kwa lugha ya Kiswahili, nacho pia kinapatikana kwenye tovuti yetu na tunawashauri wakisome,” alisema Badru.

Alisema waombaji wote wanatakiwa kuwa na vyeti vya kuzaliwa ambavyo vimethibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) huku ambao wazazi wao wamefariki dunia, wakitakiwa kuwa na nakala za vyeti vya vifo ambavyo vimethibitishwa na wakala hizo.

“Wanafunzi waliofadhiliwa na taasisi mbalimbali katika masomo yao ya sekondari au stashahada, hawa wanatakiwa kuwa na barua kutoka katika taasisi hizo. Kwa wanafunzi wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu, wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu wao kutoka kwa waganga wakuu wa wilaya au mikoa,” alisema Badru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles