28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ma-RC, DC wana wajibu wakuzalisha ajira

OFISI ya Waziri Mkuu imeeleza kwamba sekta rasmi inachangia nafasi za ajira kwa asilimia 13.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alipozindua Kampeni ya Mkoa Wetu, Viwanda Vyetu alieleza kuwa utafiti walioufanya umeonyesha tatizo la ajira bado kubwa.

Wakati Jenista akitoa taarifa hiyo mwaka juzi, idadi ya viwanda ilitajwa kuwa ni 49,000 hadi mwaka 2016 na kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, asilimia 0.85 ni viwanda vidogo vidogo, asilimia 14 ni viwanda vidogo, asilimia 0.03 ni viwanda vya kati na vikubwa ni asilimia 0.05.

Sisi wa MTANZANIA Jumapili tunaamini kuwa idadi ndogo ya viwanda vya kutosha hapa nchini inasababisha wahitimu wa vyuo vikuu kukosa nafasi za ajira.

Pia tunasikitika kuona matunda kama machungwa, maembe, mananasi na ndizi yakiachwa yaoze mashambani katika baadhi ya mikoa kwa kukosa wateja wa uhakika huku maduka makubwa yakiwa yamejaa vinywaji baridi kutoka nje ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, tunawashauri wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie

jukumu kubwa la kutengeneza ajira zenye staha katika maeneo wanayoyasimamia.

Pia tunaamini kwamba, namna bora ya kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini ni kujenga viwanda kwa sababu ndivyo vitakavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo kama pamba, kahawa, chai, korosho, kokoa, mahindi, maharage, ndizi, mananasi na aina zote za matunda.

Ndiyo maana tunaunga mkono agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, la kuwataka wakuu wa mikoa kujipima utendaji wao kwa kuhakikisha wanajenga viwanda.

Pia kampeni iliyozinduliwa na Jenista iwe kama ilani nyingine kwa watendaji hao ili kuchagiza maendeleo ya viwanda kwa nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.

Tunawashauri wakuu wa mikoa na wilaya watambue kwamba uwapo wa viwanda utawahakikishia wakulima soko la uhakika la mazao yao na hivyo kuondokana na tabu wanayopata sasa hivi.

Kwa sababu Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, imekuja na mkakati wa kukuza viwanda ili bidhaa nyingi zitengenezwe ndani ya nchi na kuuzwa nje kwa nia ya kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Kwa sababu namna ya uhakika ya kukuza na kulinda ajira ni ujenzi wa viwanda vitakavyotumia bidhaa zinazozalishwa hapa hapa nchini hususan zile zinazotokana na kilimo.

Pia tunashauri kuwa ahadi ya Serikali kutoa zawadi kwa mikoa na halmashauri tatu zitakazofanya vizuri katika upatikanaji wa viwanda iwe kama chachu ya kuwaongezea ari na maarifa viongozi hao wapate msukumo zaidi katika ujenzi wa viwanda na hivyo kukuza ajira za maana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles