MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara ya kushtukiza Kituo cha Polisi Stakishari Dar es Salaam kufuatilia utendaji kazi.
Aliwasili kituoni hapo saa 6:16 mchana wa juzi ambapo alikutana na wananchi mapokezi ya kituo hicho ambao walifika kuwachukulia dhamana ndugu zao waliopo katika mahabusu ya kituo hicho, na aliwahoji kama wanapata huduma nzuri kutoka kwa askari wa kituo hicho.
Akiwa katika mapokezi ya kituo hicho, alikichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo akiwahoji kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kuwahoji mahabusu hao, alisema ziara yake ni ya kawaida ya kufuatilia utendaji kazi wa vituo vya polisi, pia kufuatilia ahadi zake ambazo alizitoa bungeni kufuatilia vituo mbalimbali vinavyolalamikiwa.
“Lengo la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi nchini, sijaja kumwadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali kilichonifanya hapa nije nikufuatilia maagizo mbalimbali ambayo niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” alisema Lugola.
Aliwataka makamanda wa polisi mikoa mbalimbali nchini kusimamia utendaji kazi bora na kuhakikisha maagizo yake anayoyatoa yanafanyiwa kazi ipasavyo, na ataendelea kuyafuatilia na endapo yakipuuzwa hatamvumilia mtu.