MWANDISHI WETU-Dodoma
MBUNGE wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM), amesema kuwa suala la kukosekana kwa elimu ya kumwandaa mwanafunzi ni dalili mbaya kwa taifa.
Kutokana na hali hiyo, alisema sasa umefika wakati kwa Serikali kuangalia namna bora ya kutoa elimu ya kumwandaa mwanafunzi pamoja na kuangalia mitaala ya elimu kama inakidhi vigezo vya elimu na ikiwezekana ifanyiwe maboresho.
Kauli hiyo aliitoa juzi bungeni Dodoma, alipokuwa akichangia mjadala wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kishimba alisema kuwa alishtushwa na taarifa ya watu 40,000 kuwasilisha maombi ya ajira 70 zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivi karibuni.
Alisema suala hilo linapaswa kuisikitisha, kuiogofya na kuishangaza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na vyuo vikuu kwa sababu kama waombaji ni 40,000 na wanaopata kazi ni 50 hawa wengine wanakwenda wapi.
“Elimu yetu hii tulirithi kutoka kwa wakoloni Waingereza, haina pingamizi. Waingereza wakistaafu watu 900,000, watakaomaliza shule au ‘University’ (chuo kikuu) watakuwa milioni moja, kwa hiyo 900,000 watapata kazi hawa 100,000, Serikali inaweza kuwatunza na kuwahifadhi, lakini kwetu wanaomaliza shule wanaweza kuwa milioni moja wanaopata kazi ni 50,000.
“Kwahiyo tukiendelea na utaratibu huu mwenyekiti tunatengeneza bomu kubwa, kwenye suala hili naona kila mtu anaogopa kupasema, lakini ukweli mwenyekiti ni vizuri tukubaliane na Wizara ya Elimu ambao wao ndio watunga sera za elimu, iundwe kamati au tume ambayo itachunguza suala la elimu kwa Tanzania.
“Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amejaribu kuliongelea hili suala mara mbili mara tatu, lakini naona watu hawalichukulii uzito, lakini mwenyekiti watu 40,000 kama wangekuwa Uwanja wa Taifa wakasema hawatoki mle uwanjani, utakuwa na kazi ngumu ya kuwatoa,” alisema Kishimba.
Kutokana na hali hiyo, alishauri kutungwa sera mpya ya elimu itakayowawezesha kujifunza shughuli za biashara, kilimo na ufugaji badala mfumo uliopo sasa ambao mwanafunzi anahitimu elimu ya juu kwa kupewa cheti ambacho hakimwezeshi kupata ajira popote.
Kishimba alisema mfumo huo unapaswa kuhakikisha kuwa asilimia 50 ya maksi wanafunzi wazipate katika masomo hayo na asilimia 50 zitokane na masomo ya darasani.
Alisema mfumo huo utamsaidia mwanafunzi pale anapohitimu masomo yake ya sekondari au chuo kikuu, akiambiwa akajitegemee anakuwa na sababu ya msingi ya kufanya hivyo kwa sababu atakuwa akifahamu akajitegemee vipi.
“Lakini leo kumwambia mtu mwenyekiti aende akajitegemee, wewe umechukua fedha zake za ‘University’ alafu wewe ukampa unayosema ni digrii, lakini kiukweli umempa karatasi, ni sawa sawa na mtu amecheza Deci, hii digrii hakuna mahala inapotambuliwa popote, hata kama unaumwa huwezi kuiweka dhamana famasi, huwezi kuiweka dhamana benki, sasa inawezekana kweli?
“Mimi nimesomesha mtoto wangu, nimeuza mifugo yangu, nimelipa milioni 10, wewe umenipa digrii halafu wewe unaniacha mimi nikazunguke mtaani na ile digrii.
“Mimi mwenyewe ni mwathirika wa hizo digrii, ninao watoto sita wana digrii, kwa kweli mwenyetiki inahuzunisha sana, ingekuwa bora watunga sera tukubaliane kwamba vyuo vikuu kabla havijatangaza nafasi za shule zikatafute ajira zenyewe, zieleze na mishahara, ziseme tumepata NBC mshahara ni Sh 800,000, tumepata NSSF Sh 500,000, sasa tunaanza kusajili, leta milioni tano nikupe digrii kazi hii hapa,” alisema.
Alisema suala hilo linaweza kuonekana kama la kuchekesha, lakini hali ni mbaya mitaani kwa sababu watu wanazo digrii kila kona, hawana ajira.
“Lakini muda wa kusoma vilevile watunga sera waangalie. Ni nani alifanya ‘research’ kwamba ubongo wa binadamu unahitaji kila mwaka darasa moja, kama yupo atwambie. Wakati huu nafasi za ajira hakuna unachukuliwa mtoto wako miaka 17, unarudishiwa ana miaka 25 mnaambiwa katafuteni kazi ya kujitegemea, mnajitegemeaje mwenyekiti?
“Lakini kama watakubali watunga sera mwaka mmoja wasome madarasa matatu au manne ili watu wamalize shule mapema, itatusaidia sana ili mtu akimaliza shule arudi huku tuje tuendelee na maisha kijana akiwa bado mdogo. Leo wanakaa naye muda wote wanakuja kukurudishia wewe ana miaka 25.
“Ukienda kwenye familia zilizoathirika kwenye suala hili la elimu ukasema elimu ni ufunguo wa maisha watasema hapana elimu ya Tanzania ni kifungo cha maisha, maana ni kifungo kigumu, umefungwa wewe, amefungwa mtoto, amefungwa mama na fedha zimeenda, wote mna vyeti viko ukutani na majoho ya siku ya ‘graduation’, cha kufanya hamna mnatazamana,” alisema mbunge huyo.
Alidai kuwa lengo lake si kubeza elimu, lakini ni lazima yafanyike mabadiliko makubwa na kwamba nchi nyingi duniani zina matatizo kama hayo ikiwamo Afrika Kusini kwa sababu wao pia wamefuata mfumo huo wa elimu wa Uingereza ambao unakwenda kwa mfumo wa sukuma, sukuma, sukuma na kupewa cheti, lakini hakuna kitu wanachokipata.
Alisema kwa sasa wanapokwenda kwenye majimbo vijijini wakiuliza ni mtoto gani ana faida kati ya aliyesoma na ambaye hajasoma, wanajibu kuwa ambaye hajasoma ndiye mwenye faida kijijini, anayefuata wa darasa la saba, kisha wa kidato cha nne ndiyo anafuata wa chuo kikuu.
Alidai kuwa wananchi wanasema mhitimu wa chuo kikuu ni kama viazi vilivyoshindwa kuiva kwa sababu hawezi kufanya kazi yoyote ikiwamo kulima, anabaki kusubiri ajira ambazo hazipo.
“Kama zimetangazwa nafasi 50 walioomba ni 40,000 na hawa ndio wana e-mail na internet, je ambao hawana e-mail na internet na walioghairi. Je, watu hawa wako wapi sasa hivi na wanafanya nini?” alihoji.
Alisema kuwa waziri amekuwa akisema anaboresha elimu, lakini hajui ni elimu ipi inayoboreshwa kwa sababu waliohitimu hawajapata kazi.
“Bidhaa inaboreshwa pale ambapo bidhaa uliyopeleka sokoni wateja wamesema tunataka bidhaa ya aina fulani. Ukisema unataka kuboresha elimu, unaboresha ipi kama watu walio bora hawajapata kazi,” alisema.