WASHINGTON, MAREKANI
ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, amejiunga rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia kwenye chama chake cha Democratic, huku akirusha kombora kuwa Marekani itakuwa hatarini iwapo Rais Donald Trump atashinda tena kwenye uchaguzi ujao.
Katika video iliyotumwa kwenye ukurasa wa Twitter, Biden amesema Marekani imo kwenye mapambano ya kuenzi misingi ya taifa hilo na hatakubali kuendelea kutazama ikivurugwa na utawala wa Trump.
Biden mwenye umri wa miaka 76, ni miongoni mwa wagombea wenye nafasi nzuri ya kupitishwa ndani ya chama hicho pamoja na Seneta Bernie Sanders wa Jimbo la Vermont ambaye anaongoza kwenye kura za maoni.
Biden lazima atachuana na wagombea wengine wapatao 20 ndani ya chama chake ambao wanawania kumkabili Trump katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Kwa upande wake, Rais Donald Trump amemrushia kijembe Joe Biden kwa kusema kuwa ni mtu mwenye kulala sana. Akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, amesema: “Joe Biden mwenye usingizi mwingi, karibu kwenye mchuano.”
Hata hivyo, Trump ameonyesha wasiwasi wake kutokana na uwezekano wa Biden kuibuka mshindi kwenye uteuzi wa mapema wa ndani ya Chama cha Democrat kutokana na uelewa alionao makamu huyo wa zamani wa Rais wa Marekani.