ELIYA MBONEA-ARUSHA
WATU wawili wamefariki dunia na watano kujeruhiwa kutokana na ajali ya gari iliyokuwa ikiendeshwa kwa mwendo kasi kuwahi nyama choma eneo la Oldonyosambu nje ya mji wa Arusha.
Ajali hiyo ilitokea juzi eneo la Oldonyosambu wilayani Arumeru mkoani Arusha ikihusisha magari madogo mawili yenye namba za usajili T 612 DNE na KCH 665 G yaliyobeba watu saba. Wawili kati yao walifariki dunia papo hapo.
Majeruhi aliyelazwa Hospitali ya Seliani Ngaramtoni, Halmashauri ya Arusha, Anold Twahil alisema kwa kawaida huwa kuna mkusanyiko kutoka maeneo tofauti na kuendesha magari kwa kasi kisha huchoma nyama pamoja.
“Huwa tuna mchezo wa kuchezea magari, baada ya hapo tunakula nyama choma.
“Wakati tukio hilo linatokea sijui kilichotokea kwani nilikuwa nje, nilisikia mlio wa gari nikalala chini mara gari likaniangukia.
“Sikumbuki kama magari yaliyopata ajali yalikuwa kwenye tukio ambalo huwa linatukutanisha watu kutoka maeneo tofauti,” alisema Twahil.
Akizungumzia tukio la ajali hiyo jana akiwa Kituo kidogo cha Polisi Oldonyosambu, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mkoa wa Arusha, Joseph Bukombe alisema madereva wa gari hizo hawakuchukua tahadhari.
“Tunawaelimisha madereva kuendesha mwendo wa kawaida, hawa hawakuchukua tahadhari ya kuendesha watu watano, haiwezekani ‘rim’ zipasuke kama wangekuwa mwendo wa kawaida.
“Mwenye gari namba za Kenya KCH 665 G alikuwa mbele ameonyesha kukata kulia, kuelekea Ngarenanyuki eneo maarufu kwa nyama choma, eneo hilo raia wengi wa Kenya wanapendelea sana kwenda hapo.
“Gari ya Mtanzania ilikuwa nyuma ikiwa mwendo kasi na hakuchukua tahadhari kwamba eneo lile lina wananchi, kwa hiyo akawa amekuja mazima ndiyo kisa cha kuipiga ubavuni mara ikaanguka mara tatu,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Arusha, Petro Mboya, alithibitisha kupokea majeruhi watano huku wawili kati yao wakiwa na majeraha ya kichwa na wengine kwenye uti wa mgongo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, alisema hapakuwa na mashindano ya magari kama ilivyoripotiwa awali badala yake watu hao walikuwa kwenye mambo yao.
“Magari mawili yakishindana huwezi kuita hayo ni mashindano ya magari, ukweli ni kwamba walikuwa kwenye haraka haraka zao za kuwahi nyama choma ambayo hata hawakuifikia,” alisema Kamanda Shana na kuongeza:
“Tumepita hospitalini na kuwaona majeruhi kwa ujumla hali zao ni mbaya sana hasa wawili.”
Kamanda Shana aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Onesmo Mwangi raia wa Kenya na Erick Fabrique mpigapicha wa Moshi Mjini.
Waliojeruhiwa ni Robin Allan, Robin Kurya, Stella Mwigae, Rajabu Mhesa, Anold Twahil, Shadrack Anold na Bosco Mshanga.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Murro aliyewatembelea majeruhi hospitalini hapo jana, alisema juhudi zinaendelea kunusuru maisha yao.