BAMAKO, MALI
RAIS wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita, jana alikubali ombi la kujiuzulu Waziri Mkuu Soumeylou Boubeye Maiga na Baraza lake zima la Mawaziri, kutokana na maandamano ya umma dhidi ya mauaji yaliyofanyika huko Ogossagou, ambako takribani wachungaji 160 kutoka jamii ya kabila la Fulani walipoteza maisha wiki nne zilizopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Al Jazeera, vifo vya watu hao vinatajwa kufanywa na watu wa jamii ya Dogon wanaoishi kwa kilimo na uwindaji.
Mauaji hayo yaliitikisa Mali, ambayo Machi mwaka huu yalifanyika mengine kadhaa, yakiwamo ya wanajeshi 23 walioshambuliwa kwenye kituo chao.
Kabla ya uamuzi huo wa kujiuzulu, Bunge la nchi hiyo lilijadili uwezekano wa kura ya kutokuwa na imani na serikali kutokana na mauaji hayo na pia kushindwa kuwanyang’anya silaha na kuwazuia wanamgambo wa itikadi kali. Umoja wa Mataifa una zaidi ya wanajeshi 16,000 nchini Mali, vikiwamo vikosi kutoka Ufaransa na Ujerumani.
“Waziri Mkuu mpya anatarajiwa kutangazwa muda mfupi ujao na serikali mpya itaundwa mara baada ya majadiliano ya makundi yote ya kisiasa, kutoka chama tawala na vyama vya upinzani,” ilisema taarifa ya Ikulu ya nchi hiyo.
Bunge la nchi hiyo pia lilipendekeza zoezi la kuwanyang’anya silaha makundi yote ya kipiganaji yanayomwaga damu nchini humo.
Vyombo vya dola nchini Mali vimewakamata watu watano ambao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya yaliyofanyika huko Ogossagou.
Wachambuzi mbalimbali wameikosoa Serikali ya Mali pamoja na vyombo vya dola kushindwa kuzuia machafuko ya mara kwa mara yanayotokea nchini humo.
“Hali ilivyo hairidhishi kiusalama ndani ya nchi yetu. Maisha ya wananchi wa kawaida yanazidi kuwa mabaya. Bei ya bidhaa muhimu zinazidi kupanda, kama vile maji, umeme, vyakula, mwaka jana bei zilifikia asilimia 20. Waziri mkuu alichaguliwa mwezi Agosti akiahidi kuleta mabadiliko kwa wananchi wa Mali, lakini hali imekuwa tofauti na ahadi,” alisema mwandishi wa Al Jazeera, Nicolas Haque.
Mapema mwezi huu, maelfu ya wananchi waliandamana na kushiriki kwenye kampeni za kumshinikiza waziri mkuu ajiuzulu.
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya wafanyakazi 16,000 wamepelekwa nchini Mali, pamoja na askari 12,418 kutoka nchi za Burkina Faso, Senegal, Niger, Togo na Chad, kwa lengo la kusaidia ulinzi nchini humo.
“Watoto wetu, waume zetu na wazazi wetu wanakufa kwa sababu ya uongozi mbaya wa Ibrahim Boubacar Keita na kizazi chake. Hii inatosha, hatuwezi kuendelea kuongozwa na utawala huu,” alisema mjane Mariam Fomba, ambaye mumewe aliyekuwa askari alifariki dunia wakati wa maandamano.