27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi ateseka miaka mitatu kitandani kwa madai ya kuvunjwa mgongo na mwalimu

ELIZABETH KILINDI-NJOMBE

ALIYEKUWA Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Madeke, Hosea Manga (10), mkazi wa Kijiji cha Madeke Kata ya Mfriga wilayani Njombe, anadaiwa kupigwa na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu na mwalimu anayetajwa kwa jina la Focus Mbilinyi, miaka miwili iliyopita na kusababishiwa kuvunjika uti wa mgongo.

MTANZANIA Jumamosi lilifika nyumbani kwa mtoto huyo aliyekuwa akisoma darasa la tatu Kijiji cha Madeke, umbali wa kilomita 103 kutoka mjini Njombe.

Akizungumza na gazeti hili mtoto huyo alisema tukio hilo lilitokea Machi 21, mwaka 2017, akiwa na umri wa miaka (8) ambapo alipigwa na mwalimu kwa sababu ya kukosa hesabu.

Alisema siku ya tukio akiwa darasani kwenye kipindi cha somo la hesabu lililokuwa likifundishwa na mwalimu aliyemtaja kwa jina la Focus Mbilinyi ambaye aliwataka kufanya majaribio, yeye na wenzake wawili walikosa hesabu zote 10.

“Ilikuwa asubuhi tukiwa darasani tunasoma somo la hesabu mwalimu alitupa hesabu 10 na akasema ukikosa utachapwa kulingana na hesabu ulizokosa, hivyo mimi nilikosa hesabu zote na kutakiwa kuchapwa fimbo 10, mwalimu wakati anatuchapa tulikuwa watatu, alituning’iniza kichwa chini miguu juu katika moja ya dirisha la darasani ndipo nilipoangukia mgongo na kuhisi maumivu makali yaliyosababisha hadi leo natumia muda mwingi nikiwa hapa kitandani,” alisema Hosea.

BABA AZUNGUMZIA MATESO YA MWANAWE

Akizungumzia tukio hilo baba mzazi wa Hosea Manga, Boniface Manga, alisema wakati tukio hilo linatokea alichelewa kupewa taarifa na kwamba alizipata baada ya kufika shuleni hapo kwenda kuonana na mwanawe mkubwa.

“Wakati nafika pale shuleni nilikuta walimu wapo nje, wawili wakiwa kama wana uoga hivi mmoja akiwa amenyong’onyea kabisa tukasalimiana, halafu mmoja akaniambia tangu asubuhi tulikuwa tunahitaji kumweleza mzazi fulani lakini tukawa tunaogopa kumweleza kwa sababu na wewe ni mzazi, tunahitaji utueleze kama mtoto wako Hosea Manga amefika mwenyewe kutoka nyumbani kuja shuleni? Nikasema ndiyo, kama asingekuwa amefika kaka yake angesema ambaye anaongozana naye kila siku,” alisema Manga.

Manga alisema: “Wakasema inawezekana mtoto wako alikuwa mlemavu na wewe ulikuwa hujui kama mtoto huyu ni mlemavu, tumeona tukueleze sasa kwamba mtoto wako ni mlemavu,” nikawauliza taarifa za ulemavu zinatoka wapi maana mwenye kuthibitisha ni daktari nyinyi mmezitoa wapi? Wakasema sisi tunakueleza, nikataka kujua mazingira na hali iliyompata mwanangu.

“Nikawaambia walimu wale nahitaji sasa kumwona mtoto wangu na mnieleze ni sababu gani zimesababisha mchelewe kunijulisha mapema wakati anazidiwa? Akaja mwalimu mmoja hivi akitokea nyumbani naye akauliza yule mtoto amezidiwa saa ngapi? Lakini hapakuwa na jibu la kuridhisha, mwalimu wa darasa akaingia nikamweleza kuwa nahitaji kumwona mtoto maana sasa tunamchelewesha kwa sababu hamkunieleza wakati mtoto anazidiwa haina maana ya kuendelea kupoteza muda.

“Kweli nikaingia hadi darasani nikamkuta mtoto hali si nzuri, wakati ninaingia nikamwona akiwa ameegemea kwenye dawati nikasimama mbele yake ndipo walimu wakamwambia mtoto hebu inuka, wakamuuliza unamwona nani mbele yako, akasema namwona baba, hebu inuka akashindwa, tikisa mguu kwenda mbele na kurudisha nyuma akashindwa, basi ikabidi pale wamwinue katika mabega nikaona kiuno   kinazunguka na mguu wa kulia nikawaambia huduma ya kwanza mmechelewesha ndio maana hali imefikia hapa,” alisema Manga.

“Baada ya hapo nikatafuta pikipiki ya kutupeleka zahanati, lakini nilipitia kwa mwenyekiti wa kitongoji basi nikamwambia na nikaomba pikipiki akakubali na vijana wawili nikaongozana nao kwa ajili ya ushahidi nisiende peke yangu, basi tukaenda pale tukaingia darasani tukamchukua mtoto na kumpeleka zahanati ya kijiji baadaye  kituo cha afya Lupembe,” alisema.

Alisema matibabu ya mtoto huyo yaliendelea katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe, Hospitali ya Rufaa Kibena pamoja na ile ya Misheni ya Ikonda iliyopo wilayani Makete ambapo kote huko matibabu yake yalishindikana na hivyo kufikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Alisema wakati anahangaika na matibabu hayo alikuwa amefungua kesi Mahakama ya Mkoa wa Njombe na licha ya jitihada zote alizokuwa anaendelea nazo lakini alidai kuwa Chama cha Walimu Wilaya ya Njombe kilimshawishi aifute kesi hiyo ili waone namna ya kumsaidia lakini yeye alikataa.

CHAMA CHA WALIMU

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Njombe, Shaban Ambindwile, ili kuzungumzia madai hayo ambapo  alisema majukumu ya chama hicho ni kumtetea mwalimu akipata matatizo ikiwamo kumwekea wakili na kukana kama walishawishi kesi hiyo ifutwe.
“Nimefanya jitihada nyingi sana ili kumsaidia mwanangu, nimekuwa nikienda mjini mara kwa mara tangu mwaka 2017 kuonana na wanasheria bila ya mafanikio kama unavyoona umbali huu, dawa zenyewe tunanunua mjini tumepoteza kila kitu ila tunachohitaji sasa ni haki kutendeka,” alisema Manga.

Alisema kesi hiyo ya Jinai namba 83 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa nayo baadaye ilifutwa kutokana na daktari aliyemtibu mtoto huyo mara ya mwisho katika Hospitali ya Muhimbili kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane.

MAMA: TUMEPOTEZA KILA KITU

Akizungumzia tukio hilo mama wa Hosea Manga, Veronica Kipanyura, alisema wakati tukio linatokea alikuwa shambani lakini wakati anarudi kuelekea nyumbani alikutana na mwalimu Mbilinyi njiani.

“Baada ya kukutana na mwalimu huyu njiani aliniuliza kama mimi ni mzazi wa Hosea, nikamwambia ndio akaniambia mtoto nimemchapa fimbo nimezizidisha kwa sababu watoto wote nilipiga viboko lakini mtoto wako hali si nzuri, kwa vile nimekutana naye njiani na wakati huo mtoto sijamwona nikajua labda kaumia kawaida lakini nilipomwona sikuamini,” alisema Veronica.

Veronica aliongeza kuwa tangu mwanawe huyo apatwe na mkasa huo kila kitu kimesimama kwa kuwa muda mwingi wanatumia kumhudumia.

“Tulikuwa tunalima lakini sasa tumesimama, tumeuza mali ikiwemo mashamba ili mtoto apate huduma lakini hakuna tulilofanikiwa,” alisema.

Alisema baada ya kesi hiyo kufutwa walikubaliana na familia kwenda kupeleka malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, kwa ajili ya kupata msaada.

MKUU WA MKOA

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Ole Sendeka, ambaye alikiri kupokea malalamiko hayo.

Ole Sendeka aliomba atafutwe wakati mwingine ili aweze kutoa maelezo yaliyojitosheleza.

“Sina mengi ya kukwambia, nimesikia habari ya huyo mtoto ila naomba nitafute baada ya shughuli ya ziara na hawa wageni,” alisema Ole Sendeka akiwa na haraka ya kuwahudumia wageni waliofika ofisini kwake.

MTANZANIA Jumamosi bado linaendelea kumtafuta Mkuu huyo wa Mkoa ili aweze kutoa kile alichokiita yeye mwenyewe kuwa ni maelezo yanayojitosheleza.

KAULI YA MWANASHERIA WA SERIKALI

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Wakili Helman Danda, alikiri kesi hiyo kufutwa kwa sababu Jamhuri ilishindwa kupeleka shahidi ambaye ni daktari wa mwisho aliyemtibia mtoto huyo Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli nimefuatilia nimeona kesi ilifutwa na sababu ni upande wa ushahidi ambaye ni daktari wa Muhimbili kushindwa kuja kutoa ushahidi, kwa mazungumzo zaidi mtafute Mkuu wa Mkoa,” alisema Danda.

MWENYEKITI WA KIJIJI

Mbali na Ole Sendeka, Mwenyekiti wa Kijiji cha Madeke, Dikrey Kilula, alilithibitishia gazeti hili kutokea kwa tukio hilo na kwamba jitihada walizochukua kama kijiji ni kwenda kufungua kesi mahakamani.

“Hakuna siri kila mtu hapa kijijini aliona kilichotokea kwa sababu watoto waliokuwa na Hosea darasani walienda kutoa ushahidi, lakini hatujui huko mahakamani kilitokea nini, mtoto anateseka, shule ameacha kwa sababu ya hali yake na pia mwalimu aliyefanya tukio hili alihamishwa,” alisema Kilula.

MWENYEKITI WA BODI YA SHULE

Juhudi za gazeti hili kumtafuta Mwalimu huyo ambaye inasemekana amehamishiwa Kata ya Mtwango zinaendelea baada ya mara kadhaa kutopatikana.

MTANZANIA Jumamosi halikuishia hapo lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Madeke, Gadi Ndangarasi, ambaye alisema kuwa alimkuta Hosea shuleni akiwa hawezi kusimama akiwa amelemaa kwa sababu ya kuchapwa viboko na mwalimu.

“Nilipokaa kikao na walimu ndani waliniambia alikuwa akiadhibiwa viboko na mwalimu Mbilinyi na baada ya kuadhibiwa ndio hali hiyo ikamtokea, tukampeleka zahanati ambako alionekana hali si nzuri kwamba kama vile ameadhibiwa viboko vingi,” alisema Ndangarasi.

Kwa sasa mtoto Hosea anatumia muda wake mwingi akiwa amelala kitandani  kutokana na maumivu makali anayoyapata baada ya kutokewa na tukio hilo la kuumia mgongo lililosababisha kutokea kwa kidonda kikubwa sehemu ya chini unapoishia uti wa mgongo.

Zaidi wakati wote wa ugonjwa wa takribani miaka miwili, ameshindwa kuendelea na shule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles