27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Programu ya ‘Madaraka Mikoani’ ilizorotesha huduma za jamii

HILAL K SUED

HISTORIA ya Serikali za Mitaa katika nchi hii baada ya uhuru inashabihiana sana na hali ya sasa ilivyo katika halmashauri hizo aliyoirithi Rais John Magufuli.

Bado ni mapema mno kufahamu iwapo hatua yake ya kuihamisha wizara inayosimamia halmashauri hizo (TAMISEMI) kuitoa ofisi ya Waziri Mkuu na kuiweka chini ya ofisi yake itatatua chanagamoto kubwa inayozikabili halmashauri nyingi nchini tena kwa muda mrefu – changamoto ya ufisadi uliokuwa umekithiri.

Halmashauri za wilaya na zilizokuwapo katika baadhi ya miji baada ya uhuru ziliendelezwa hadi mwanzoni mwa miaka ya 70 pale serikali ya Mwalimu Julius Nyerere ilipozifuta ili kupisha kile kilichoitwa ‘madaraka mikoani’ (decentralization) – programmu ambayo haikuwa imeeleweka sawasawa. Unafuta serikali za mitaa halafu unaita madaraka mikoani?

Wadadisi wa mambo wanasema hapo ndiyo ilikuwa mwisho wa muda mfupi wa Utawala Bora na wa uwajibikaji katika utendaji kazi wa serikali uliokuwapo na kuwa mwanzo wa uchafu wote ambao Serikali ya Kikwete iliwahi kudhamiria kuuondoa lakini ikashindikana na sasa Magufuli naye anajaribu kwa namna yake.

Na ninadhani ni vyema nikaeleza tu hapa kwamba ile sera ya ‘madaraka mikoani’ na suala la utaifishaji wa majumba mwanzoni mwa miaka ya 70 zililenga kuwadanganya tu wananchi kujisikia kwamba wao ndiyo wamiliki wa mali za nchi na utawala pia. Tusisahau kwamba utaifishaji majumba haukuwamo katika ilani (blueprint) ya Azimio la Arusha ya umilikaji wa njia kuu za uchumi iliyotangazwa mwaka 1967.

Utaifishaji wa majumba ulikuja baada tu ya mapinduzi ya kijeshi nchini Uganda mapema 1971 yaliyoongozwa na jenerali Idi Amin na ambayo kwa namna moja au nyingine yalisababisha mawimbi hapa nchini. Rais Julius Nyerere aliona kama vile anazidiwa kete na Idi Amin katika suala la kuwawezesha kiuchumi wazalendo wa nchi yake.

Kwani baada tu ya kutwaa madaraka, Idi Amin alitangaza kuwafukuza watu wenye asili ya Kiasia waliokuwa na paspoti za Uingereza ambao ndiyo walikuwa wanashikilia uchumi na biashara nchini humo. Alinyang’anya mali zao pamoja na shughuli zao za kibiashara na kuwapa wazawa.

Utaifishaji wa majumba

Hivyo Nyerere aliona naye lazima afanye kitu na hivyo kabla ya ‘madaraka mikoani’ ikaja sheria ya utaifishaji wa majumba ambayo mengi yalikuwa yakimilikiwa na watu wa asili ya Kiasia ili Watanzania wajisikie sasa ni ya kwao. Lakini hata hivyo wapangaji wakubwa wa majengo hayo waliendelea kuwa watu wa jamii hiyo ya Kiasia na Waafrika wazalendo walikuwa wakienda kwenye magorofa hayo kama watumishi wa ndani na kwenye maduka yao kununua mahitaji.

Kwa upande wake sera ya madaraka mikoani iliiathiri sana nchi kwa sababu masuala ya kiutawala katika wilaya na maeneo ya miji hasa katika utoaji wa huduma muhimu za jamii zilianza kuzorota tena kwa kasi.

Badala ya kuwa na madiwani waliochaguliwa na wananchi kulikuwapo kamati za maendeleo za wilaya zilizokuwa zinafanya kazi za mabaraza ya udiwani na zilizoundwa na wakuu wa idara mbalimbali za wilaya hizo pamoja na makada wengine wa chama (TANU) wote wakiwa chini ya Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya(ma-DDD) na ambao nao walifanya kazi chini ya maelekezo ya Wakuu wa Wilaya, (Area Commissioners). Hawa wakuu wa Wilaya na ma-DDD walikuwa wanateuliwa na Rais. Wote hawa walifanya kazi za ‘udiwani’.

Hata hivyo mpango huo haukuhusu maeneo ya miji ambayo shughuli zake za kiutawala zilikuwa chini ya wilaya husika, ila tu kwa Jiji la Dar es Salaam ambalo lilikuwa na Meya na Mkurugenzi wa Jiji, wote wakiwa wateule wa Rais.

Na wakati huo huo kulikuwapo mfumo wa ‘kofia mbili’ ambapo wakuu wa wilaya na wa mikoa pia walikuwa wakuu wa chama tawala katika maeneo yao. Katika mfumo huu, uwajibikaji ulipotea kutokana na kutokuwapo kwa mgawanyo halisi wa madaraka ulioeleweka na hivyo watendaji kutupiana mpira katika kutoa uamuzi na uwajibikaji.

Kama nilivyosema huduma za jamii ziliporomoka hasa katika miji na hakuna aliyekuwa anajali na/au kuwajibika kwa lolote lililokuwa likienda ovyo katika maeneo husika.

Hatimaye Serikali ilizinduka

Hali iliendelea kuwa mbaya hadi mwanzoni mwa miaka ya 80 ambapo serikali ilizinduka na kuona sera ya madaraka mikoani haifai na kilichobaki ni kurejea kwa mfumo wa zamani wa utawala wa halmashauri, mfumo unaotumiwa na zaidi ya asilimia 95 ya nchi zote duniani.

Miaka kumi ilipotea bure katika kufanya majaribio ya mfumo ambao malengo yake hasa hayakuwa yamewekwa wazi. Isitoshe mfumo huu wa sasa ulirejeshwa wakati nchi ilikuwa inapita wakati mgumu sana kiuchumi kwani ilikuwa tu ndiyo imeibuka kutoka vita iliyotugharimu sana.

Hata hivyo halmashauri zilizorejeshwa hazikuwa za aina ile ya zilivyokuwa kabla ya miaka ya 70. Ziliendeshwa na makada wale wale wa chama kwani chaguzi zake (pamoja na zile za Wabunge) zilipambanisha baina ya makada wawili wa chama hicho hicho na kuwafanya wapigakura wachague mmoja wao – kutumikia sera na ilani ile ile iliyowekwa na chama.

Hivyo kwa miaka 12 iliyofuatia halmashauri hizi ziliendeshwa kwa namna ya ‘majaribio’ kwa mara ya pili tena na ilitokana na maelekezo ya chama kwani madiwani waliweka chama mbele kabla ya wananchi kwa hofu ya kutoteuliwa tena kugombea. Ni kama vile ilivyokuwa kwa wabunge tu.

Kidogo hali ya uwajibikaji ilirudi baada ya ujio wa mfumo wa ushindani wa vyama vingi ambao uliwezesha wagombea kutoka vyama mbalimbali kushindana katika chaguzi za madiwani.

Lakini, kama usemi maarufu wa Kiingereza  unavyosema ‘Old habits die hard’- yaani tabia za zamani zilizozoeleka huwa ngumu kuondoka. Chama tawala kiliongoza asilimia kubwa sana ya halmashauri nchini, lakini katika zile chache ambazo wapinzani waliziongoza, serikali ilianza tabia ya kuzinyima ruzuku kwa kile kinachoweza tu kuhusishwa na masuala ya siasa. Lengo ni kuonesha kwamba wapinzani hawawezi kuleta maendeleo kwa wananchi.

Hali ya namna hii iliendelea hasa kutokana na vyama vya upinzani kuongoza halmashauri nyingi zaidi, hasa zile muhimu za miji, likiwamo ile ya Jiji la Dar es Salaam.

Kama nilivyotaja hapo juu Rais Magufuli aliihamisha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) – wizara inayosimamia halmashauri zote kutoka ofisi ya Waziri Mkuu na kuiweka chini yake (Ofisi ya Rais). Lengo bila shaka ni kujaribu kudhibiti utendaji wa halmashauri hasa kutokana na masuala ya ufisadi- saratani ambayo imekuwa ikishamiri bila vizuizi vyovyote vya maana.

Udhibiti wa Halmashauri za upinzani’

Lakini katika ‘udhibiti’ huo bila shaka ataangalia kwa jicho la pili zile halmashauri zinazoongozwa na wapinzani. Tayari tuliona figisufigisu zilizotokea wakati wa uchaguzi wa mameya katika halmashauri kadha nchini hususani za Dar es Salaam –Ilala, ile iliyokuwa ya Kinondoni, na ya Jiji.

Kulikuwapo jitihada za chinichini (zilizoshindikana) kwa upande wa chama tawala kulazimisha kupitishwa kwa wateule wa chama hicho kuwa mameya.

Kama ni kudhibiti ufisadi katika halmashauri ni bora Rais Magufuli akafanya hivyo bila kujali ni chama gani kinaongoza halmashauri na aende zaidi ya kile alichodhamiria mtangulizi wake Kikwetwe.

Tukumbuke kwamba si mara moja au mbili Kikwete alitishia kuzifuta halmashauri ambazo hazikuwa zinafanya vizuri kiutendaji kutokana na ufisadi na utafunaji fedha. Hakuifuta hata moja.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles