Majambazi wameng’oa mashine ya kielektroniki ya kutolea pesa (ATM) nchini Ireland.
Majambazi hao walitumia tingatinga ambalo pia waliliiba katika kufanikisha tukio hilo la kung’oa mashine hiyo kutoka kwenye ukuta wa duka moja katika Kaunti ya Antrim.
Polisi wamethibitisha kuwa jengo lilikuwa na mashine hiyo limeharibiwa vibaya baada ya majambazi kutoa mashine hiyo na kutokomea nayo kusikojulikana.
Mmiliki wa duka hilo Walter Millar amesema kuwa ATM hiyo “itakumbukwa sana” na jamii ya eneo hilo na sasa kuna “hofu” juu ya kupatiwa mashine nyengine baada ya wizi huo.
Awali alipopokea taarifa juu ya wizi huo, mmiliki wa duka hilo bwana Millar alidhani ni uzushi tu wa Siku ya Wajinga, Aprili mosi.
“Nachoweza kusema ni kuwa, wametumia tingatinga ambalo waliliiba kwenye eneo moja la ujenzi mwishoni mwa mtaa, wakainyofoa mashine na kuipakia kwenye gari na kuondoka nayo,” amesema.