MGOMBEA urais wa Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein amesema maendeleo kwa wafanyabiashara wadogo visiwani humo ni lazima.
Kutokana na hali hiyo, ameahidi kuwajengea eneo la maonyesho ya biashara ili kuwavutia wafanyabiashara wa nje.
Akizungumza katika viwanja vya Urafiki, Jimbo la Sahurimoyo mjini Unguja juzi, Dk. Shein alisema mradi huo licha ya kuwavutia wafanyabiashara, utawasaidia kutangaza biashara zao.
“Wafanyabiashara wadogowadogo ndiyo wanaofanya biashara wengi, hatuwezi kuwatupa au kuwanyanyasa, tuwajengee uwezo madhubuti, tayari Serikali imeanza mazungumzo na watu mbalimbali kuhakikisha wanatimiza azma ya ujenzi wa eneo hilo.
“Nitahakikisha ujenzi huu,unakamilika mapema kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yakiwamo mifuko ya hifadhi ya jamii na benki zetu,” alisema.
Alisema miaka mitano ijayo, atazidisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo.