GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana ametangaza kurudi rasmi chama alichokuwa awali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitokea Chadema alikokaa kwa takribani miaka mitatu.
Lowassa aliihama CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kupitisha mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015, ambapo Rais John Magufuli alisimamishwa na kushinda.
Shughuli ya kumpokea Lowassa jana ilifanyika Ofisi Ndogo ya CCM, Makao Makuu, Lumumba, jijini Dar es Salaam na iliongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. Magufuli.
Rais Magufuli, ambaye alikuwa sambamba na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na baadhi ya makada wa chama hicho, akiwamo Rostam Aziz, alisema Lowassa amerudi nyumbani.
“Ndugu
zangu kama alivyozungumza, Lowassa, ametumia maneno mafupi, amerudi nyumbani na
nyumbani ni hapa CCM, ndiyo maana amesimama kwenye jengo la Makao Makuu Ofisi
ndogo ya CCM,” alisema Rais Magufuli.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru alipozungumza, alisema Lowassa ametangaza
kurudi nyumbani na wamempokea.
“Ametangaza kurudi nyumbani na tuko tayari kumpokea,” alisema Dk. Bashiru.
Itakumbukwa kuwa kabla ya jana kurudi CCM, Lowassa alijiunga na Chadema Julai 2015, baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mchakato wa kutafuta mgombea wa urais ndani ya CCM.
Lowassa alikihama CCM na kwenda Chadema akiongozana na baadhi ya wanachama na madiwani waliokuwa wakimuunga mkono na hivyo kusababisha mtikisiko kwa chama hicho.
Baada ya Lowassa kuingia Chadema, aliteuliwa kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao ni muunganiko wa vyama vya upinzani, kikiwamo CUF na NCCR-Mageuzi.
Kutokana na kuungwa mkono na wengi, hususan vijana, Lowassa alitoa upinzani mkali kwa Rais Magufuli katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015.
Katika matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Rais Magufuli alipata kura 8,882,935, ikiwa ni asilimia 58.46, huku Lowassa alijipatia kura 6,072,848, ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.
Baada ya upepo wa siasa hizo za uchaguzi kupita, Januari 2018, kupitia mtandao wa Chadema kulikuwa na barua ambayo ilisainiwa na Lowassa na kueleza kuwa alikutana na Rais Magufuli na kufanya mazungumzo ambayo yalimtaka kurejea CCM.
Katika majibu yake, Lowassa alisema alimjibu Rais Magufuli kuwa uamuzi wake wa kukihama CCM kwa wakati huo haukuwa wa kubahatisha.
Kutokana na uamuzi wa jana wa Lowassa kurejea CCM, MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene, ili kupata kauli ya chama hicho ambapo alisema mwanasiasa huyo ametumia haki yake kikatiba.
“Ametumia haki yake kikatiba. Tunamtakia kila la kheri huko aendako,” alisema Makene.
Mwisho