30.4 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Rais al- Sisi atazingatia mapendekezo ya Kagame?

Othman Miraji

Kati ya watu sita duniani, mmoja anaishi katika Bara la Afrika, na thuluthi moja ya wakimbizi au watu waliofukuzwa makwao wako Afrika. Wakati Wazungu wana wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokea mawimbi makubwa ya wakimbizi kutoka Afrika kumiminikia Ulaya, lakini ukweli ni kwamba asilimia 90 ya kutangatanga wakimbizi kunatokana na kuukataa ukweli mwingine, ambao huen da kwa baadhi ya watu ni mchungu, kwamba Afrika ni Bara la Wahamiaji.

Umoja wa Afrika, AU, katika mkutano wake wa kilele uliomalizika karibuni katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwa mara ya kwanza uliliingiza rasmi suala la ukimbizi na kutangatanga watu ndani ya nchi za Afrika katika ajenda ya mazungumzo yake. Umoja huo uliutangaza mwaka huu wa 2019 kuwa Mwaka wa Wakimbizi, kurejea wakimbizi hao makwao pamoja na watu waliofukuzwa kutoka maeneo yao ndani ya nchi zao.

„Mimi mwenyewe nilikuwa mkimbizi kwa miaka minane ya maisha yangu“, ameelezea Rais wa Komisheni ya AU, Moussa Faki Mahamat wa kutokea Chad, katika hotuba yake ya kuufungua mkutano huo. Mgeni katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisifu kwamba: licha ya changamoto za kijamii, kiuchumi na kiusalama zilioko barani Afrika, serikali na watu wa Afrika wameacha wazi mipaka, milango na mioyo yao kwa watu wanaozikimbia shida na kuwa katika mahitaji. Alisema Afrika imeonesha vipimo vya juu kabisa kudhihirisha mashikamano yao kwa watu walio katika mashaka.

Wahamiaji na wakimbizi wanaweza wakawa ni utajiri kwa nchi inayowapokea, hivyo si lazima waangaliwe kuwa ni mzigo. Wageni hao wepya huziimarisha nchi zinazowapokea. Mfano ni nchi mbili za Bara la Afrika: Uganda na Ethiopia ambazo zimewapa wakimbizi haki ya kufanya kazi punde wanapowasili katika nchi hizo. Uganda imekuwa ikifanya hivyo kwa muda mrefu, nayo Ethiopia imeanza kufanya hivyo tangu 2018.

Nchi hizo mbili zinaongoza katika kupokea wakimbizi kwa wingi sana katika Afrika, licha ya ya hatari ya kufanya hivyo. Waeritrea wanaokimbia kutoka serikali ya kidikteta ya nchi yao hukaribishwa Ethiopia, kama vile wanavyokaribishwa watu wanaovikimbia vita vya kienyeji katika Sudan Kusini. AU pia ina makao yake makuu Addis Ababa.

Mwaka jana serikali ya Morocco ilipewa jukumu na AU itunge siasa ya Afrika kuelekea uhamiaji, na mwaka huu ripoti juu ya siasa hiyo iliwasilishwa mbele ya Mkutano wa Kilele wa Addis Ababa. „Suala la uhamiaji lazima liwekwe katika msingi wa matarajio ya maendeleo“, ilisema ripoti hiyo ya Mfalme wa Morocco. Sababu zinazopelekea uhamiaji- kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, kukosekama utulivu wa kisiasa na mapigano baina ya makabila- ni vitu vya kupambana navyo, lakini ukimbizi na uhamiaji haifai tena kuchukuliwa kuwa ni kitisho au hatari kwa usalama. Pia vitu hivyo si kitisho kama vile nchi za Ulaya zinavyopendelea kushauri kwa nchi za kiafrika.

Kila serikali ya Kiafrika inatambua kwamba katika siku za mbele kutakuweko uhamiaji zaidi, wala si kidogo. Kutoka idadi ya sasa ya watu bilioni 1.2, ifikapo mwaka 2050 idadi ya wakaazi wa Afrika itaongezeka na kufikia bilioni 2.5, na wakati „watu wengi wanaiona hali hiyo kuwa ni kitisho, kwetu sisi tunaiona kuwa ni nafasi“, alisema waziri wa mambo ya kigeni wa Morocco, Mohcine Jazouli, huko Brussels mwezi Januari mwaka huu.

Katika makisio yake ya uchumi kwa mwaka 2019 iliowasilisha mbele ya Mkutano wa Kilele wa AU, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilitaja kwamba: hadi Januari 2030 vijana milioni 295 wataingia katika masoko ya ajira katika Afrika. Hiyo ni nyongeza ya asilimia 40 ya vijana wenye kuweza kufanya kazi. Hivi sasa kuna tu nafasi milioni 12 mpya za kazi. Benki hiyo imeonya kwamba hadi 2030 yawezekana vijana milioni 100 wakawa hawana ajira.

Vijana hao watafanya nini ikiwa hawana ajira? Kati ya malengo ya muda mrefu ujao, Mkutano wa Kilele wa AU ulitaka Waafrika waweze kusafiri baina ya nchi zote za Afrika vila ya ulazima wa kuwa na viza na pia kuweko biashara huru baina ya nchi za kiafrika. Ni hapo

uhamiaji ndani ya Afrika litakuwa ni jambo la kawaida kama ilivyo huko Ulaya.

Kabla ya kuja wakoloni wa Kizungu Afrika haijawa na mipaka baina ya nchi na nchi kama ilivyo sasa. Tutumai kwamba pale ile kasumba ya mabaki ya ukoloni wa Kizungu itakapotoweka kabisa pia mipaka iliyochorwa na Wazungu baina ya nchi na nchi nyingine ya Kiafrika itapotea, mistari iliotenganisha jamii za kaka na dada wa ukoo mmoja itaondoka. Hapo tena Afrika itakuwa imeshinda kuachana kabisa na mabaki ya ukoloni wa kigeni na kuweza kujitambua upya yenyewe.

Uhamiaji baina ya nchi za Kiafrika, kama ni wa hiyari au wa kulazimishwa, ni jambo la kawaida katika historia ya Afrika. Jamii nyingi za kiafrika za hivi sasa zimejengeka kwa mtindo huo. Mtu yeyote katika Afrika anayezuwia kuhamahama kwa watu, basi atambue kwamba anawazuilia watu wao mustakbali wao, tena huenda ukawa mzuri kabisa.

Rais Abdelfattah al-Sisi wa Misri alichaguliwa kuwa kiongozi wa AU kwa mwaka huu akichukua nafasi alioyokuwa akiishikilia Rais Paul Kagame wa Rwanda. Katika hotuba yake mbele ya mkutano huo wa Addis Ababa al-Sisi hajatwama juu ya suala la ukimbizi na uhamiaji- mada muhimu ya mkutano wa mara hii- lakini alisisitiza juu ya lengo la AU kwamba hadi ifikapo mwaka 2020 matumizi ya silahayasite kote barani Afrika. Alishikilia kwamba njia ya hadi kufikia jambo hilo bado ni ndefu.

Katika kipindi chake cha urais wa AU, Paul Kagame aliiongoza AU ishughulikie masuala hasa ya kuleta mageuzi ndani ya umoja huo. Alikuwa na makusudio ya kuifanya AU iwe na uwezo mkubwa zaidi, hasa ijitegemee yenyewe kifedha. Alipendekeza idadi ya makamishna wa AU ipunguzwe na alifaulu kuzifanya hadi sasa nusu ya nchi wanachama 55 wa AU ziukubali msingi wa kuchangia katika bajeti ya AU- kila nchi mwanachama ichangie asilimia 0.2 ya thamani ya bidhaa inazoagizia kutoka nje ya Afrika. Pindi jambo hili litatekelezwa basi kwa mara ya kwanza AU haitotegemea kifedha kutoka nje ya Afrika.

Al-Sisi, lakini, anatawala kwa mabavu huko Misri. Na tangu alipoingia madarakani miaka minne sasa amekuwa akitumia njia za kikatili kupambana na wapinzani wake wa kiliberali na wale wenye siasa za Kiislamu wa Chama cha Udugu wa Kiislamu(Muslim Brotherhood). Jeshi lake limekuwa likitumia silaha kupambana na watu anaowaita magaidi katika eneo la Sinai. Si hasha kipaumbele kwake kikawa ni usalama, na atataka AU ifuate mwelekeo huo.Al-Sisi si mshabiki wa mageuzi yaliopendekezwa na Kagame; pia atautilia nguvu msimamo wa nchi yake ya Misri katika mabishano yake na nchi zinazopakana na Mto Nile- kama vile Ethiopia- juu ya matumizi ya maji ya mto huo.

Al-Sisi hatakuwa kama Kagame, hatokuwa tayari kuzilaumu serikali za nchi nyingine za Afrika. Wiki chache zilizopita AU, kutokana na ushawishi wa Kagame, kwa njia rasmi, ilijizuwia kuyatambua matokeo ya uchaguzi ya nchi mwanachama. Hali hiyo ilitokana na mabishano kufuatia ushindi wa mwanasiasa wa upinzani, Felix Tshisekedi, katika Uchaguzi wa Congo. Kuna wahakiki waliodai kwamba ushindi wa Tshisekedi katika uchaguzi huo ulikuwa wa kugushi kwa lengo la kuyahifadhi maslaha ya rais aliyetangulia, Joseph Kabila.

Hata hivyo, AU haijafuata kuchukua hatua yeyote baadae. Tshisekedi alipokelewa kama mgeni wa heshima katika Mkutano wa Kilele wa Addis Ababa, na zaidi ya hayo akachaguliwa kuwa makamo wa pili wa rais wa AU.

Makamo wa Kwanza wa Rais wa AU ni Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini- na ambaye pindi atashinda uchaguzi wa urais nchini mwake mwaka huu- atamfuata al-Sisi mwaka 2020 kuwa kiongozi wa AU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles