WASHINGTON, MAREKANI
IKULU ya Marekani imekataa kuzungumzia uwezekano wa kuwepo mkwamo mwingine wa shughuli za serikali kutokana na kuwapo mvutano mpya kuhusu wahamiaji.
Mvutano huo unahusu iwapo kuna haja ya kuweka viwango vya idadi ya wahamiaji, ambao maofisa waandamizi wanaweza kuwazuia kuingia Marekani, kikiwa kizungumkuti kingine kuhusu usalama mpakani.
Kwa sasa, Chama cha Republican cha Rais Donald Trump na mahasimu wao Democratic, bado vinavutana kuhusu kiasi cha fedha kinachohitaji kutumika kufadhili mpango wa Trump wa kujenga ukuta katika mpaka kati ya Marekani na Mexico.
Mvutano huo umesababisha kutopitishwa bajeti ya shughuli mbalimbali na hivyo kuzikwamisha.
Muda wa mwisho wa muafaka kupatikana kuhusu suala hilo ni Ijumaa wiki hii, la sivyo Marekani itashuhudia tena mkwamo wa shughuli za serikali.