29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri waagizwa kukagua ujenzi wa majengo ya wizara

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza mawaziri wafike katika maeneo ya ujenzi wa ofisi zao, watathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara na watakapojiridhisha ni mdogo, wawabadilishe mara moja.

Agizo hilo alilitoa jijini hapa jana baada ya kukutana na mawaziri 15, manaibu waziri na makatibu wakuu katika eneo la tenki la maji la kutolea huduma katika ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba badala ya Ukumbi wa Hazina kama alivyokuwa amepanga awali.

“Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu hapa saiti ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati,” alisisitiza.

Pia aliwapa mrejesho mawaziri juu ya changamoto alizokutana nazo juzi alipofanya ukaguzi wa ujenzi kwa kila wizara. “Nataka Mawaziri ambao ofisi zao zinajengwa wa watu wa Mzinga wakae nao na kutathmini uwezo wao na kama mtaona hawawezi, mkabidhi kwa mkandarasi mwingine,” alisema.

 Aliwataka wakandarasi wahakikishe wanaongeza idadi ya vibarua ili kazi hiyo iweze kwenda haraka. “Wizara iliyofanya vizuri kuliko zote ni ya Utumishi, wao wako hatua nzuri. Kwa maana ya uchapaji kazi, eneo nililokuta lina wafanyakazi wengi ni magereza,” alisema.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alimweleza Majaliwa kwamba kuna wagongaji wa kokoto walipokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.

“Waziri wa Madini aongee nao hawa watu ili warejee na kufanya kazi kwa sababu baadhi yao wameshapokea fedha na mahitaji ya kokoto hapa ni makubwa na aliyebakia akifanya kazi ni Nyanza Road Works peke yake,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alimweleza Majaliwa kwamba wizara yake imetoa transfoma tisa za kusaidia kupoza umeme lakini ni wizara nne zilizojitokeza na kulipia laini za transfoma hizo.

“Wizara yetu tumetoa transfoma tisa za kusaidia umeme upatikane eneo la ujenzi. Niwaombe mawaziri waliopo, walipie service laini tu ambazo gharama yake ni shilingi 921,000 ili wafungiwe transfoma na kazi iweze kufanyika mchana na usiku.

“Hadi sasa, tumeshapokea maombi kutoka wizara nne tu za Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati ili kazi imalizike ndani ya muda mfupi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles