30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Ndugulile: Wanawake jitokezeni chanjo ya mabusha

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya kumeza dawa ya kinga ya magonjwa ya minyoo ya tumbo,usubi, trakoma, matende na mabusha katika mikoa saba hapa nchini. Kushoto ni Mratibuwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Dk. Upendo Mwingira.
 VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM

WANAWAKE pia wamehimizwa kujitokeza kumeza dawa kinga dhidi ya matende na mabusha kwa sababu  hata wao wapo katika uwezekano wa kuugua ugonjwa huo kama ilivyo kwa wanaume.

Imeelezwa kuwa miaka iliyopita wazee walishindwa kuchomekea mashati maarufu ‘kuulambia’ kutokana na kupata mabusha huku jamii ikielewa hali hiyo inasababishwa na kurogwa.

Dhana nyingine iliyokuwa inatajwa kwenye jamii ni umwinyi huku wengine wakidhani hali hiyo husababishwa pia  na kunywa maji ya madafu jambo ambalo si kweli.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile.

Alikuwa  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya kunywesha dawa kinga ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, usubi, trakoma, matende na mabusha.

“Kuwa na busha si umwinyi, ni ugonjwa, hausababishwi na kunywa maji ya madafu wala si wa kurogwa, unasababishwa na minyoo ambayovimelea vyake huenezwa na mbu wa aina zote,” alisema.

Alisema mabusha huweza kuwapata pia wanawake ingawa huwa ni mara chache mno kama ilivyo kwa wanaume.

Alisema ndiyo maana wizara imejikita kuwakinga wananchi kwa kuwapatia dawa kinga hizo, lengo ni kuvunja mnyororo wa maambukizi.

“Lengo kuu la kampeni  ni kutibu na kuzuia maambukizi ya magonjwa haya, dawa hizi zitasaidia kupungua kwa ulemavu na adha za magonjwa haya.

Dk. Ndugulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni alisema dawa kinga hizo zinatolewa katika mikoa saba nchini.

“Zitatolewa Dar es Salaam katika Manispaa zote, Songwe katika Manispaa ya Songwe, Irnga (Mufindi), Mtwara (Masasi), Pwani (Kibaha na Mafia), Rukwa (Kalambo), Tanga (Mkinga na Korogwe).

” Kuna faida kubwa kwa wananchi wakishiriki katika kumeza dawa kinga hizi, ikiwamo kukinga upungufu wa damu, kumuepusha mtu kupata upofu, kupunguza maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda mwingine, kuua vimelea vya magonjwa hayo.

“Kukinga na kupunguza maumivu na madhara yanayosababishwa na magonjwa haya, kupunguza magonjwa ya ngozi, kuongeza virutubisho bora mwilini, kuboresha nguvu kazi katika jamii, kuwezesha watoto kukua vizuri na kuongeza uelewa wa watoto wanapokuwa  shuleni.

“Lengo ni kutibu na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, usubi, tracoma, matende na mabusha (ngirimaji).

“Dawa hizi zitasaidia kupungua kwa ulemavu na adha za magonjwa haya,” alisema.

Alisema tangu serikali ilipoanzisha kampeni hiyo ya kumeza dawa kinga mafanikio yamepatikana na yamedhibitiwa katika manispaa 98.

“Tumefikia pazuri, zimebaki manispaa 28 tunataka Tanzania tutokomeze matende na mabusha, mwaka 2013 watu wapatao 3,028,828 walijitokeza na kupatiwa kinga tiba, 2017 watu 4,914,351 sasa na asilimia 86 yalengo lililotarajiwa na mwaka huu wanatarajiwa kumezesha watu 5,376,207,”alibainisha.

 Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Dk. Upendo Mwingira, alisema mwaka jana wanaume 1,000 walifanyiwa upasuaji na kuondolewa mabusha.

“Kuna   wanaume 4,000 katika Mkoa wa Dar es Salaamambao wanasubiri huduma ya upasuaji, mwakani tumepanga kuanzia Wilaya ya Kigamboni,” alisema.

Alisema kuhusu matende hakuna tiba ya upasuaji zaidi ya kumuelekeza mgonjwa jinsi ya kusafisha sehemu iliyopata tende iwe ni mguuni, mkononi au kwenye ziwa.

“Jambo la msingi tunasisitiza wananchi wajitokeze kupata dawa kinga dhidi ya magonjwa haya,” alisema Dk. Mwingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles