ANDREW MSECHU
MHANDISI wa Kampuni ya Mask and Sons ya jijini Dar es Salaam, Leonard Mkaka, amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za rushwa ya ngono, huku dereva mmoja akihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja ama kulipa faini ya Sh 300, 000 kwa kosa la kumpa askari wa barabarani rushwa ya Sh 5,000.
Katika taarifa ya wali, iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Pilly Mwakasege, Mkaka alikamatwa juzi saa saba mchana katika nyumba ya wageni iliyopo Kibada, Kigamboni akiwa na mlalamikaji, tayari kwa kutekeleza azma yake.
Mwakasege alisema waliamua kumfuatilia mtuhumiwa huyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mlalamikaji ambaye alidai kuombwa rushwa ya ngono na mhandisi huyo ili amuwekee daraja (culvert) kwenye nyumba anayoishi.
“Mlalamikaji alikuwa ameomba awekewe culvert kufuatia miundombinu ya barabara kuelekea nyumbani kwake kuharibika kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea katika eneo hilo,” alisema.
Alisema ombi hilo lilifikishwa kwa mtuhumiwa ambaye ni mhandisi wa kampuni hiyo iliyopewa jukumu la kutengeneza miundombinu ya barabara na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, katika Kata ya Tuangoma Mtaa wa Masaki.
Alisema mtuhumiwa alianza kuomba rushwa ya ngono kwa mlalamikaji (jina limehifadhiwa) kuanzia Novemba 16 hadi Desemba 4 mwaka huu, alipokamatwa na maofisa wa Takukuru ambao walikuwa wakimfuatilia na kukusanya ushahidi katika kipindi hicho chote.
Mwakasege alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka chini ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11 ya mwaka 2007 mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Katika tukio jingine, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Luzango Khamsin amemhukumu kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh 300,000 dereva wa gari aina ya Noah, Rashid Ally Katunda kwa kosa la kutoa rushwa ya Sh 5,000 kwa askari wa usalama barabarani.
Kwa mujibu wa mashitaka, Dereva Rashid ambaye hufanya safari zake katika barabara kati ya Mikumi na Ifakara, alimpa rushwa askari Polisi E.6993 CPL. Elvis aliyekuwa akitekeleza majukumu yake katika barabara ya Ifakara – Morogoro ili asichukuliwe hatua za kisheria kwa makosa ya usalama barabarani ya kutokuwa na leseni ya udereva pamoja na uchakavu wa bodi ya gari yaliyokuwa yanamkabili.
Taarifa ya Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Janeth Machulya iliyothibitishwa na Msemaji wa Takukuru, Dorice Kapwani jana, Katunda alikamatwa na maofisa wa Takukuru Januari 29, 2018 na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero ambapo alifunguliwa Kesi ya Jinai Namba 14/2018.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Ainainyi Minja aliielezea Mahakama kuwa Katunda anashtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 kama hati ya mashtaka ilivyofafanua.
Aidha, baada ya upande wa mashtaka kutoa ushahidi pasi na shaka, Mwendesha Mashtaka aliiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na wengine wanaotenda makosa kama hayo.