NA PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, kwa madai ya kuidharau mahakama na kukiuka masharti ya dhamana waliyopewa katika kesi ya msingi iliyokuwa inawakabili.
Kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.
Washtakiwa hao kwa pamoja walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka 13, yakiwamo ya kufanya mikusanyiko, vurugu na maandamano yasiyo halali na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.
Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, alisema licha ya mahakama hiyo kutoa dhamana kwa washtakiwa wote, Mbowe na Matiko wameidharau mahakama kwa kukiuka masharti ya dhamana waliyopewa.
Kutokana na hali hiyo, alisema mahakama imeamua kuwafutia dhamana washtakiwa hao wawili na waliobaki wataendelea na dhamana zao.
Hakimu Mashauri alisema washtakiwa hao wawili, Novemba mosi na Novemba 8 mwaka huu, walishindwa kufika mahakamani bila kutoa sababu za msingi.
Alisema katika maelezo yake, Mbowe alisema kwamba aliondoka nchini Oktoba 28, kuelekea Washington DC, Marekani kuhudhuria mkutano uliofanyika Oktoba 30 na Oktoba 31, usiku alipotaka kurejea nchini kwa ajili ya kusikiliza kesi yake, aliugua ghafla.
Alisema Mbowe alieleza kuwa baada ya kushambuliwa na ugonjwa, alishauriwa asisafiri umbali mrefu kwa ndege lakini hati yake ya kusafiria inaonyesha alisafiri umbali mwingine mrefu kwa ndege, jambo linaloonyesha kwamba alikuwa anadharau amri za mahakama kwa makusudi.
“Jambo hilo ni uongo kwa sababu katika hati yake ya kusafiria ilionesha kuwa alisafiri kutoka Marekani Novemba 2, alikwenda Brussels nchini Ubelgiji huku akitakiwa kufika mahakamani Novemba mosi mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza kesi yake.
“Licha ya Mbowe kueleza kuwa alitakiwa kupumzika, lakini nyaraka yake ya matibabu ilionesha kuwa Novemba 8, ndio alipata matibabu Dubai kwenye nchi za Falme za Kiarabu (UAE), wakati akijua alitakiwa kufika mahakamani,” alisema.
Alisema haiwezi kuingia akilini kwamba daktari alizuia mshtakiwa kuruka na ndege kutokana na ugonjwa wake huku akienda nchini Ubelgiji ambako alikaa kuanzia Novemba mosi hadi 6 na kusafiri tena kwenda Dubai kwa ajili ya matibabu.
Kutokana na hali hiyo, alisema anaungana na upande wa mashtaka kwamba Mbowe hakwenda kwenye mkutano badala yake alikuwa na safari zake binafsi ndipo akapata ugonjwa huo.
Alisema lakini pia mdhamini wake aliidanganya mahakama kuwa Mbowe alienda Afrika Kusini akiwa mahututi na hakuweza kuongea.
Alisema suala la Mbowe kusafiri kwake kwa muda mrefu inaonesha kuwa ameidharau mahakama kwa kuzungumza mambo ya uongo.
Akizungumzia kuhusu mshtakiwa Matiko, Hakimu Mashauri, alisema nchi inaongozwa na sheria na ni matakwa kwamba mshtakiwa akikabiliwa na makosa ya jinai pamoja na vyeo vyao bado wanatakiwa kuwepo mahakamani.
“Maelezo aliyoyatoa Matiko kwanini asifutiwe dhamana hayakidhi matakwa ya yeye kushindwa kuhudhuria mahakamani wakati kesi ilipokua itakuja kwa ajili ya kutajwa, alikua analeta dharau.
“Mahakama imeamua kuwafutia dhamana zao mshtakiwa wa kwanza na wa tano (Mbowe na Matiko) na kurudishwa mahabusu,” alisema.
Alisema sababu alizozitoa Matiko kuwa alihudhuria ziara ya kibunge nchini Burundi si za msingi na hazikidhi matakwa ya kutofika mahakamani.
Katika kesi hiyo, upande wa utetezi uliongozwa na wakili, Peter Kibatala, huku upande wa Serikali ukiongozwa na mawakili, Faraja Nchimbi na Paul Kadushi, Simon Wankyo na Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainab Mango.
Mara baada ya kutoa uamuzi huo, Wakili Kibatala, alidai kuwa wana kusudio la kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo chini ya kifungu cha 161 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 20 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kifungu hicho kinaeleza kuwa amri zote za dhamana zinaweza kukatiwa rufaa au kufanyiwa marejeo Mahakama Kuu.
Hata hivyo, mawakili wa Serikali waliiomba mahakama hiyo kuendelea na hatua ya usikilizwaji na kwamba wana mashahidi wapo tayari kuendelea.
Hoja hiyo ilipingwa na Wakili Kibatala ambaye aliiomba mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo kwa sababu hawako tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo na kwamba mahakama ijielekeze kuwapatia nakala ya uamuzi.
Alidai washtakiwa wana haki ya kupeleka rufaa Mahakama Kuu hivyo wanataka mchakato uanze mara moja ili kuipeleka mahakamani.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Nchimbi alidai hoja za ahirisho zinakosa sapoti za sheria na taratibu kwani mara ya mwisho shauri hilo lilipokuwa linaahirishwa, mahakama ilisema inaahirishwa kwa ajili ya uamuzi na kuendelea na usikilizwaji.
Alidai masuala yanayohusiana na dhamana ni tofauti na kusikilizwa kwa kes hiyo, hivyo Mahakama itupilie mbali maombi hayo na iruhusu kuendelea kusikilizwa.
Mara baada ya mabishano ya kisheria, Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi saa 7:30 mchana jana, ili aweze kutoa uamuzi wa kuendelea na kesi hiyo au la.
Wakati kesi hiyo ilipoahirishwa, Wakili Kibatala, alifungua maombi ya dhamana Mahakama Kuu ambayo yanasubiri kupangiwa tarehe ya kuanza kutajwa.
Ilipofika saa 7:30, Hakimu Mashauri alisema upande wa washtakiwa umefungua rufaa ya maombi ya dhamana kwa wateja wao kwa sababu ni haki yao ya msingi.
Alisema wakati rufaa hiyo ikiendelea katika Mahakama Kuu, washtakiwa hao wataendelea kukaa mahabusu mpaka uamuzi utakapotolewa.
“Baada ya upande wa washtakiwa kufungua kesi ya rufaa ya kupinga uamuzi wa kuwafutia dhamana, washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu mpaka uamuzi utakapotolewa na Mahakama Kuu,” alisema Hakimu Mashauri.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 6, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa huku Mbowe na Matiko wakienda mahabusu.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo inaendelea, mshtakiwa Heche hakuwepo mahakamani hapo kwa sababu anauguliwa na mkewe ambaye amefanyiwa upasuaji mdogo wa kujifungua na kuandika barua ya kuiomba mahakama hiyo kuendelea na kesi hata kama hayupo.