Mwandishi Wetu, Morogoro
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, ameibuka na kukikingia kifua chama hicho kuwa kinatekeleza siasa ya ujamaa na kujitegemea kwa vitendo.
Akitolea mfano moja ya utekelezaji wa vitendo wa chama hicho amesema hatua ya ya serikali kuamua kusomesha watoto bure elimu ya msingi hadi sekondari ni moja ya misingi ya siasa za ujamaa na kujigemea.
Shaka ameyasema juzi kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Open, ambapo na kuongeza kuwa anayedhani siasa ya ujamaa na kujitegemea imekufa basi atakuwa hajielewi.
“Anayefikiri Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea imekufa yeye mwenyewe hajielewi, serikali inaposomesha wanafunzi bure, kutafuta madawati, kulipa mishahara walimu, kujenga vyuo vikuu, kutafuta vifaa vya kufundishia, vitabu vya ziada na kiada, zahanati na hospitali ni utekelezaji chini ya siasa ya ujamaa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Shaka amesema Watanzania hawana ndoto ya kutaka mabadiliko ya utawala kwa kutegemea wenye mawazo duni waliokosa dira na malengo huku serikali ya CCM ikijibadili, kimfumo na kisera kukidhi matakwa ya wakati katika sekta ya elimu.