Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga kushirikiana na Bodi ya Korosho (CBT) kuweka mkakati endelevu wa soko la zao hilo kwakuwa si rahisi Serikali kuwa ndio mnunuzi kila utapofika msimu wa Korosho.
Kauli hiyo ya CUF inakuja baada ya Jumatatu Novemba 12, Rais Dk. John Magufuli kutangaza kununua korosho yote katika mikoa ya Lindi na Mtwara, huku akiliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuanza kazi ya kuisomba kupeleka kwenye maghala.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 16, Mkurugenzi wa Habari wa CUF Abdul Kambaya amesema chama chao kinaipongeza hatua hiyo ya Rais Magufuli katika kufikia lengo la kuhakikisha wakulima wa korosho sio tu kuuza bali wanauza kwa bei nzuri.
“CUF inafahamu kuwa katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli kutakuwepo na changamoto kama vile wafanyabiashara wa magodaoni, wenye magari ya usafirishaji na wabebaji wa korosho kupakia katika magari na halmashauri kupoteza tozo za ushuru lakini hoja muhimu ya iliyozusha mjadala ni maslahi ya mkulima ambayo yamezingatiwa kwa uamuzi huu.
“Bodi zetu za mazao mbalimbali zijikite sio tu kwenye usimamizi wa uzalishaji kwa maana ya kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo lakini ziwe na uwezo wa utafutaji wa masoko ya mazao yanayozisimamia,” amesema Kambaya.
Aidha Kambaya amesema wanatoa wito kwa serikali pia kutazama changamoto hizo ambazo pia zipo katika mazao ya Pamba, Kahawa, Alizeti, Chai, Ufuta, Karafuu na mazao mengine ili kujenga taswira sawia ya utatuzi kwa wakulima wote nchini.