Na Christian Bwaya
TUCHUKULIE mwanao amekuwa na tabia ya kufanya vibaya darasani. Kwa kuwa hupendi afanye vibaya unaona ni vizuri uongee naye kumhamasisha afanye juhudi kwenye masomo.
Unamwambia, “Hebu jitahidi mwanangu. Alama hizi unazopata hazifai. Mimi sijawahi kupata alama hizi. Nilipokuwa na umri kama wako, nilikuwa na bidii kwenye masomo. Kwa sababu ya kufanya bidii, siku zote nilishika nafasi kati ya nambari moja na tatu darasani.”
Lengo ni jema kabisa. Unachofikiri hapo ni kuwa mwanao akisikia simulizi ya mafanikio yako, atahamasika na kuanza kujitahidi. Unafikiri uwezo wako unaweza kumhamasisha kijana. Inawezekana ikawa hivyo. Lakini mara nyingi mambo huwa kinyume.
Unapomwambia kijana namna ulivyokuwa ukifanya vizuri, unaweza kuibua hisia mchanganyiko. Kijana wako anaweza kusikia ujumbe tofauti na huo. Kichwa chake kinaweza kuchakata taarifa tofauti kabisa. Ujumbe huo huo ukasikika: “Mimi baba yako nilikuwa mtu mwenye akili sana. Nashangaa kwanini wewe ni mjinga kiasi hiki.”
Tafsiri hiyo inafanya nafsi ya mtoto ijisikie kudhalilika. Hakuna mtu anayependa kujisikia dhalili. Ili kukabiliana na udhalili huo, mtoto anafikiri, huyu mzee anajiona kichwa sana. Hapa ameniita kunizodoa tu. Sasa nitakachofanya ni kuachana naye. Kwanza haelewi mambo yalivyo magumu shuleni siku hizi.
Kwa kawaida, watu wanavutiwa na wale wanaofanana nao; wanaoishi maisha kama yao; wenye changamoto kama zao. Hujisikia vizuri kuona mtu anayewashauri, anaelewa maisha yao, yuko kama wao.
Ni vigumu kumvutia mtu unayemwonesha ulivyo tofauti naye. Unapomfanya ajione tofauti na wewe, labda kwa kuwa na uwezo asio nao yeye, anakata mawasiliano na wewe. Akisha kata mawasiliano hayo, anawasha taa itakayomsaidia kumulika ujumbe wako kwa kuukosoa; kuubatilisha ili kuhalalisha kwanini yeye anapata matokeo tofauti na hayo unayomsimulia. Matokeo yake hawezi kufurahia kuusikiliza hata kama ujumbe wako ungemsaidia.
Nasaha na ushauri mwingi mzuri hukosa kibali kwa walengwa. Wanaoshauri hutumia nguvu nyingi kujitofautisha na wanaolengwa. Tofauti hiyo inakaribisha shughuli ya ujumbe huo kupingwa.
Mfano, mzazi anaongea na vijana wenye changamoto za uhusiano ya ujana. Pengine kwa kufikiria kwamba anaweza kuwahamasisha, anatumia muda mwingi kusimulia namna yeye alivyokuwa na ‘ujana mtakatifu.’ Vijana hawa ambao tayari hawana huo utakatifu, wanajisikia dhalili. Hawata msikiliza. Fikra zao zitakata mawasiliano na kuanza kuhoji yasiyolengwa. Watahoji ukweli wa yanayosemwa; tofauti ya mazingira ya wakati huo na haya waliyonayo waona kwa kweli uwezekano wa wao kupokea ujumbe huo ni mdogo.
Vijana hawa ambao tayari wanaishi kwenye changamoto wanahitaji mzazi mwenye ujasiri wa kwanza, kuelewa mazingira yao na waamini kuwa anaelewa. Pili, ili wamwamini mzazi huyu anahitaji kuwa na ujasiri wa kuwaambia namna yeye mwenyewe alivyokuwa kama wao lakini akajifunza kushinda changamoto hizo kama zao.
Kijana mwenye changamoto anapoyaona maisha yake kwa mzazi huyu, atafungua moyo wake kujifunza kwa vipi anaweza kuiga mbinu za kufanikiwa. Ndio kusema, upungufu, makosa na udhaifu vikisemwa vizuri vinaweza kuwa na nguvu ya kumbadilisha mtu kuliko simulizi za mafanikio.
Kwa wazazi, kama kweli unataka kijana wako ahamasike kuchukua hatua za kubadilisha tabia yake, huna sababu ya kumsimulia namna ulivyokuwa bora kuliko yeye. Mfanye ajione kwenye maisha yako. Atahamasika kubadilika.
Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Mawasiliano simu 0754870815, [email protected]