Na Kulwa Karedia – TSJ
WANAHISA wa Kampuni ya Vodacom wamepitisha uuzaji wa Kampuni ya Mirambo Holdings kwa Vodacom Group ya Afrika Kusini.
Mirambo Holdings ambayo inamiliki asilimia 26.25 ya Vodacom Tanzania, ni uwekezaji wa mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz.
Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam jana, Mkaguzi wa Hesabu za Ndani Vodacom Tanzania, Alvin Kajula alisema asilimia 88.18 ya wanahisa halali walipiga kura kupitisha uamuzi wa kuuzwa.
Kajula alisema wanahisa walipiga kura hizo katika mkutano mkuu maalumu uliofanyika Dar es Salaam jana.
Alisema thamani ya sehemu ya Mirambo katika Vodacom Tanzania kwa sasa ni Dola za Marekani milioni 200 sawa na Sh bilioni 460, lakini hakueleza ni kiasi gani Vodacom Afrika Kusini itamlipa Rostam.
Mwaka 2014, Rostam aliwauzia Vodacom Afrika Kusini sehemu ya asilimia 17.2 ya Vodacom Tanzania kwa kiasi kilichoripotiwa kuwa Dola za Marekani milioni 240. Wakati huo, Rostam alikuwa na hisa kupitia Kampuni binafsi ya uwekezaji ya Cavalry Holdings iliyosajiliwa katika Kisiwa cha Jersey nchini Marekani.
Vodacom Tanzania ambayo ina zaidi ya watumiaji milioni 11, ni kampuni kubwa ya simu za mkononi Tanzania na ya pili kwa Vodacom Group, inayofanya shughuli zake Afrika baada ya Afrika Kusini ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 23.
Agosti mwaka jana, kampuni hiyo ilijumuishwa kwa mara ya kwanza katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).
Rostam (57) aliyewahi kuwa bilionea namba moja Tanzania, licha ya hisa zake Vodacom Tanzania, alitengeneza utajiri wake kupitia Kampuni ya Madini ya Caspian, sehemu ya Bandari Dar es Salaam na uwekezaji katika vyombo vya habari.