Victor Bariety na Emanuel Ibrahim, Geita
WATU watatu wamefariki dunia na wengine 51 kujeruhiwa mkoani Geita, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupasua gurudumu kisha kupinduka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema watu walifaki dunia katika  ajali hiyo majina yao hajatambuliwa kutokana na miili yao kuharibika vibaya.
Alisema ajali hiyo, iliyotokea saa 3;30 asubuhi katika eneo la Nyantorotoro, ilihusisha basi la Sheraton lenye namba za usajili T138 AVD aina ya Scania mali ya Carib Abdalah ambayo ilikuwa inatoka Ushirombo kwenda Mwanza.
Alisema chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa, ingawa alisema taarifa za awali zinaonyesha basi hilo lilipasuka gurudumu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk. Adam Sijaona alithibitisha kupokea miili ya watatu hao na majeruhi 51 ambao wamelazwa.
Alisema kati ya majeruhi hao, wanaume ni 26, wanawake 25, watoto wawili wenye umri wa mwaka mmoja na mwingine wa miezi 6.
Alisema majeruhi nane ambao wamejeruhiwa sehemu mbalimbali, akiwamo derva  wa gari hilo, Kin Daud hali zao ni mbaya na wanafanya utaratibu wa kuwahamishia Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza.