Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa kamati Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa leo Alhamis Novemba Mosi, amefika katika kituo cha Polisi Mburahati kujua hatima ya kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anayeshikiliwa kituoni hapo.
Hata hivyo polisi walikataa kumruhusu Lowassa kumuona Zitto wakisema kuwa muda wa kumuona ulishapita.
Lowassa amesema kuwa alikwenda kujua hatma ya kiongozi huyo na kusisitiza kuwa wako pamoja naye na watahakikisha haki inatendeka.
“Huyu ni kiongozi mwenzetu huku upinzani, lazima tushikamane kukabiliana na lolote lililo mbele yetu, tunahitaji kuwa kitu kimoja kuliko wakati mwengine wowote,” alisema Lowassa.
Lowassa alifika kituoni hapo majira ya saa tisa mchana na mmoja wa wasaidizi wake alikwenda kuomba kibali cha kiongozi huyo ili amuone Zitto Kabwe lakini aliambiwa muda umekwisha.