Na Shomari Binda, Manyoni
MAOFISA watano wa Wizara ya Kilimo wamefariki dunia papo hapo baada ya gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajli STK 8925 kugongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili RAC 152 Y.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike alisema ajali hiyo ilitokea jana saa tano asubuhi katika Kijiji cha Njirii wilayani Manyoni.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, ni dereva wa gari la Serikali kujaribu kuyapita malori mawili yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua hadhari, huku akiwa mwendo kasi kitendo kilichofanya ashindwe kulimudu gari lake.
“Uzembe wa derava ndiyo umesababisha ajali hii…alijaribu kuyapita malori mawili bila kuchukua tahadhari yoyote mbele yake…tumekuwa tukikemea mwendo wa aina hii kila siku, lakini wapo madereva ambao bado wanakaidi,”alisema.
Alisema wakati dereva huyo akijaribu kuyapita magari hayo, alikutana uso kwa uso na lori ambalo lilikuwa linaendeshwa na Rubwata Kamanzi na kugongana uso kwa uso, huku gari dogo likiharibika vibaya.
Alisema lori hilo ni mali ya Kampuni ya Mount Meru,l ilikuwa likitoka nchini Rwanda kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Njewike aliwataja waliofariki dunia kuwa ni, Stella Osson (39), Esther Mutatembwa (36), Abdallah Mushumbusi (53),Charles Somi na Erasto Mhina (43).
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Njewike ametoa wito kwa maderava kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani, ili kuepuka ajali zinazosababisha Watanzania wengi kupoteza maisha yao na mali zao, huku wakiacha familia zao ambazo zinawategemea kwa mahitaji ya kila siku.
“Kwa kipindi kirefu sasa, tumekuwa tukiwaelekeza madereva wawe wa Serikali au magari binafasi kuendesha magari kwa kufuata sheria za barabarani…cha kusikitisha wapo ambao wanakiuka jambo hili linasikitisha mno”alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagita alisema amesikitishwa na vifo hivyo kwa sababu taifa limepoteza nguvu kazi iliyokuwa bado inahitajika.
“Mchango wa watumishi hawa ulikuwa bado unajitajika, ni huzuni kubwa kupoteza vijana wetu ambao naamini walikuwa kwenye safari ya kutimiza majukumu yao,”alisema.
Alisema watumishi hao walikuwa wakitokea Dodoma kwenda mkoani Mwanza kutekeleza majukumu yao.
“Natoa pole kwa watumishi wote wa Wizara ya Kilimo na Watanzania kutokana na ajali hii…tuwaombee vijana wetu wapumzike,”alisema.
Alisema katika ajali hiyo, dereva wa lori ambaye hakutambuliwa jina lake mara moja, alitoweka baada ya kutokea ajali hiyo.
Alisema miili ya marehemu wote ilisafirishwa jana jioni kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kusubiri taratibu nyingine.