Elizabeth hombo, Dar es Salaam
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limefuta matokeo ya darasa la saba katika shule zote za Halmashauri ya Chemba iliyopo mkoani Dodoma na shule nyingine nane kwa udanganyifu katika mitihani hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumanne Oktoba 2, Katibu Mkuu Necta, Dk. Charles Msonde amezitaja shule zilizofutiwa kuwa ni Shule ya Msingi Hazina na New Hazina, Alliance na New Alliance na Shule ya Kisiwani iliyopo Mwanza kwa udanganyifu katika mitihani hiyo.
“Aidha, baraza hilo limefuta vituo vyote vya mitihani ya shule hizo hadi pale baraza litakapojiridhisha, na shule zilizofutiwa matokea, mitihani hiyo itarejewa Oktoba 8 na 9 mwaka huu,” amesema Dk. Msonde.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Tixon Zunda ametengua uteuzi wa maofisa wote wa elimu katika Halmashauri kwa kushiriki katika udanganyifu huo.