Na GUSTAPHU HAULE,PWANI
Zaidi ya watu watano wamefariki dunia kwa kuliwa na mamba huku wajawazito wakijifungulia chini ya mti kutokana na kukosa kivuko katika Mto Mdimu unaotenganisha Mtaa wa Lumumba na Muheza iliyopo Kata ya Mailimoja Kibaha pamoja na Kibwegere jijini Dar es Salaam.
Matukio ya watu hao kuliwa na mamba katika mto huo yametokea katika vipindi tofauti hususani nyakati za masika ambapo mvua inaponyesha mto huo hujaa maji na hivyo kusababisha wananchi wa maeneo hayo kushindwa kuvuka kwa kuwa hakuna daraja la kudumu.
Kutokana na hali hiyo wananchi wa mitaa ya Lumumba, Muheza na Kibwegere wamelazimika kuanza kujitolea kwa kuchanga fedha kiasi cha Sh 15,000 kila mmoja kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika mto huo ambapo pia wameiomba Serikali iwasaidie katika kutatua kero hiyo.
Wakizungumza na MTANZANIA, juzi katika eneo la mto huo baadhi ya wananchi hao walisema kuwa kero ya kukosaa daraja katika mto huo ni kubwa kwakuwa maisha yao yanaendelea kuwa hatarini na hivyo kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo .
Mkazi wa Kata ya Mailimoja, Riti Albano, alisema kuwa wakati mvua inaponyesha maji hujaa kwenye mto huo na hivyo kusababisha wajawazito kujifungulia chini ya mti na wengine kupoteza maisha kwakuwa wanashindwa kuvuka mto.
Alisema wananchi wa Mailimoja wanategemea kupata huduma za kijamii katika Mtaa wa Kibwegere Kibamba na hivyo pindi mto unapojaa maji hakuna shughuli yoyote ya maendeleo zinazofanyika.
Naye Esther Hekima, alisema kuwa mwaka huu ameshuhudia jirani yake akiliwa na mamba wakati akijaribu kuvuka mto huo kwa ajili ya kufuata huduma eneo la Kibwegere jambo ambalo linaendelea kuleta mashaka kwao.
Alisema katika mtaa wao hakuna shule wala zahanati ila hutegemea huduma hizo kutoka upande wa pili wa Kibwegere.
“Sisi wananchi wa pande hizi mbili mvua inaponyesha hakuna mawasiliano yoyote kwahiyo tunamuomba Rais Magufuli ambaye ni mtetezi wa wanyonge atusaidie kupata daraja katika mto huu ili wananchi wake tuweze kuishi kwa amani kwakuwa kwasasa maisha yetu yapo hatarini,” alisema Hekima
Mwenyekiti wa kamati ya kikundi cha Lumuki kilichoundwa kwa ajili ya kuchangisha fedha na kusimamia shughuli ya ujenzi wa daraja hilo Idd Chamali, alisema kuwa kutokana na kero hiyo kuwa kubwa wananchi walilazimika kuunda umoja huo kwa haraka ili kufuatilia na kutatua kero hiyo.