25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MUSWADA KUTAKA MIGOGORO YA MIKATABA ISULUHISHWE NCHINI WATUA BUNGENI

Na ESTHER MBUSSI,DODOMA



Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ambao pamoja na mambo mengine imeainisha kuwa migogoro ya miradi ya wabia hao, itaamuliwa na vyombo vya kisheria vya Tanzania kwa mujibu wa Sheria za Tanzania.

Hata hivyo kambi ya upinzani bungeni, imeonyesha wasiawasi juu ya kifungu hicho ikisema wawekezaji wakubwa wanaamini mahakama za nje zaidi kuwa ziko huru.

Wakati  upinzani wakisema hivyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango akiwasilisha muswada huo  bungeni jana, alisema licha migogoro hiyo kuamuliwa nchini, piamuswada huo umeainisha mikataba ya PPP na marekebisho yake ni lazima ihakikiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kukubaliwa na Kamati ya maamuzi ya PPP.

Muswada huo pia umependekeza kuiondoa Kamati ya Taifa ya Uwekezaji katika masuala ya kuidhinisha miradi ya PPP kwa lengo la kupunguza mlolongo wa mamlaka za maamuzi katika usimamizi wa programu ya PPP.

Dk. Mpango, alisemam lengo la muswada huo ni kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa programu ya PPP nchini ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia utaratibu wa PPP.

Alibainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mlolongo mrefu wa michakato ya uidhinishaji wa miradi ya ubia ambao unaathiri kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa miradi ya PPP.

Changamoto nyingine ni waziri mwenye dhamana na masuala ya PPP kutokuwa na mamlaka kisheria ya kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na kanuni za PPP kwa kuwa sasa hivi sheria zinamtambua waziri mwenye mamlaka na masuala ya uwekezaji kama msimamizi wa miradi ya PPP.

MAPENDEKEZO YA MUSWADA

Dk. Mpango muswada huo unapendekeza pia kuwepo kwa faini ya makosa ya adhabu chini ya sheria hiyo kuwa isiyopungua Sh milioni tano na isiyozidi Sh milioni 50 au kifungo kisichopungua kipindi cha miezi mitatu na kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

“Aidha, Ibara ya 15, ya muswada kama ilivyorekebishwa kupitia jedwali la marekebisho inapendekeza kufanya marekebisho ya kifungu cha 28 cha Sheria ili kumpa waziri mamlaka ya kuandaa kanuni zinzotoa mwongozo wa uwezeshaji wa wazawa kiuchumi katika miradi ya PPP ikiwamo ununuzi wa bidhaa na huduma za wajasiriamali wa Tanzania, kuwapa mafunzo na teknolojia na uwajibikaji wa makampuni kwa jamii.

“Ibara ya 16 na 17 za  muswada zinapendekeza kurekebisha Sheria ya Uwekezaji Tanzania, sura ya 38 ili kurekebisha kifungu cha 5(4)(c) cha Sheria hii ili kuondoa mamlaka ya Kamati ya Taifa ya Uwekezaji ya kuhakiki miradi ya ubia iliyoidhinishwa.

“Lengo la marekebisho hayo ni kupunguza mamlaka za maamuzi katika utekelezaji wa miradi ya PPP, aidha kamati hiyo itabakia na jukumu la kutoa miongozo ya ujumla ya kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji wa miradi mikubwa,” alisema.

Alisema serikali inapendekeza kufanyiwa marekebisho kwa Kifungu cha 5, Ibara ya 5 ili kukiwezesha Kituo cha Ubia kuwa na jukumu la kuwasilisha taarifa za upembuzi yakinifu, wazabuni watakaopendekezwa na mikataba ya miradi PPP kwenye Kamati ya Kusimamia Miradi kwa ajili ya kuidhinishwa.

Alisema hatua hiyo inalenga kukabiliana na changamoto za kiutendaji katika utekelezaji wa miradi ya PPP ikiwamo mikakati ya kujenga uwezo sekta binafsi nchini kushiriki katika uwekezaji kwenye miradi ya PPP, uimarishaji wa soko la hisa na mitaji pamoja na sekta ya fedha katika kutoa mikopo ya muda mrefu.

“Ibara ya 10 ya Muswada, inapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 15 ili kumpa mamlaka waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kuruhusu baadhi ya miradi ya kipekee inayoibuliwa na sekta binafsi kutoshindanishwa, aidha, muswada umebainisha vigezo vya kuzingatiwa kwa miradi ambayo haitashindanishwa.

“Lengo la marekebisho hayo ni kuongeza wigo wa serikali kupata miradi yenye sifa inayoibuliwa na sekta binafsi lakini ambayo haihitaji mchango wowote wa kifedha au dhamana kutoka serikalini na ambayo ina manufaa mapana kwa nchi.

“Aidha, inapendekezwa kufuta kifungu cha 15(3) na kukiandika upya ili kuainisha kuwa, baada ya andiko la awali mradi unaowasilishwa na mbia atatakiwa kuweka dhamana ya kiasi kisichozidi asilimia tatu ya gharama za mradi ambacho kitarejeshwa kwa mwekezaji, lengo la hatua hii ni kupata wawekezaji makini na miradi yenye tija kwa taifa,” alisema Dk. Mipango.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene, alisema kamati yake imebaini ili miradi ya ubia iweze kufanikiwa ni lazima kuwe na nia ya dhati ya kuingia ubia ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na pili kuwepo na uelewa wa kutosha kuhusu uwekezaji kupitia njia ya ubia.

“Uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi bado ni tasnia changa nchini, hivyo kuna haja ya kuhakikisha kwamba tunajenga uwezo wa wa wataalamu watakaoshiriki katika mazungumzo na uandaaji wa mikataba kuhakikisha taifa linanufaika.

KAMBI YA UPINZANI

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema uchambuzi uliofanywa na kambi hiyo unaonyesha kwamba sekta binafsi nchini inalekea kuporomoka kwa sababu serikali imeacha kutekeleza mapendekezo Mpango ya Taifa wa Maendeleo ambao ndiyo dira inayoongoza katika miradi ya maendeleo.

Alisema mabadiliko ya sheria yanapendekeza pamoja na mambo mengine inapotokea mgogoro kati ya mbia na serikali, mgogoro husika utatatuliwa na mahakama za ndani kupitia sheria za ndani.

“Tunazipenda na kuziheshimu mahakama zetu, lakini pia ni ukweli kwamba PPP itahusisha wawekezaji wa ndani na wawekezaji wa nje, mwekezaji yeyote makini anataka kwenda katika mahakama za usuluhishi wa masuala ya kibiashara ambazo ziko ‘neutral’.

“Utaratibu huu wa kutumia mahakama za ndani pekee utawafukuza wawekezaji makini wa nje hasa kwa kuzingatia kwamba kuna miradi ambayo inatarajiwa wawekezaji watumie fedha zao wenyewe kwa asilimia 100.

“Tatizo si kutumia mahakama za nje, nchi hii imejikuta ikiingia katika madeni makubwa na kushindwa kesi kutokana na mikataba mibovu, tushughulikie tatizo na msingi na si matokeo,” alisema.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles