27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘UTORO’ WA WABUNGE WAULAZA MUSWADA SHERIA YA TLS, DAWA ZA KULEVYA

RAMADHAN HASSAN NA ESTHER MBUSSI
-DODOMA


SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambao unapendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria 13, ambapo pamoja na mambo mengine, imependekeza marekebisho ya Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambayo inalenga kumpatia Mwanasheria Mkuu wa Serikali fursa ya kuangalia kama kanuni husika zimezingatia masharti ya Sheria za nchi.

Aidha, katika marekebisho hayo, Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, Kifungu cha 4, kinampoka Waziri wa Katiba na Sheria mamlaka ya kumteua Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali badala yake imeweka masharti uteuzi huo ufanywe na Rais.

Hata hivyo, muswada huo ulishindwa kupita baada ya akidi ya wabunge kwa ajili ya kuupigia kura muswada huo kutotimia.

Akiwasilisha muswada huo jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema madhumuni ya muswada huo ni kuimarisha utendaji wa taasisi za Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuondoa mwingiliano wa majukumu ya kitaasisi.

Alisema madhumuni mengine ni kuhuisha miundo ya baadhi ya taasisi ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi za serikali lakini pia ili kuendana na mabadiliko ya sheria yaliyotokea katika sekta hiyo.

SHERIA YA TLS
Akizungumzia Sheria ya TLS, Profesa Kabudi alisema katika marekebisho ya sheria hiyo pia vimewekwa vigezo ambavyo vitatumika kuwapata Wajumbe wa Baraza na taratibu za kufuatwa wakati wa utungaji wa kanuni zinazosimamia chama hicho.

“Sehemu ya 14 ya muswada wa marekebisho ya Sheria ya TLS, Sura ya 307, imeweka masharti ya kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzipitisha kanuni zinazotungwa na Baraza la chama hicho kabla ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali,” alisema.

SHERIA YA MAKOSA YA JINAI, DAWA ZA KULEVYA
Katika sheria hiyo Profesa Kabudi alisema inapendekezwa Kifungu cha 57, Sura ya 20 ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, kuongeza masharti yatakayowezesha wapelelezi na wachunguzi kufanya mahojiano kwa kutumia vifaa vya sauti au vya kidijitali ambapo Jaji Mkuu atatunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti hayo.

“Kifungu cha 188 cha Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, kinarekebishwa kwa lengo la kuainisha masharti yanayotoa ulinzi kwa mashahidi wanaoitwa kutoa ushahidi wao mahakamani, iwapo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), atafungua maombi kwa ajili hiyo.

“Ulinzi unaotajwa kwa sasa katika sheria hiyo ya sasa unahusu kutotaja majina yao kwenye magazeti.

“Muswada unapendekeza pia kufanya marekebisho ya kifungu cha 205 cha sheria hiyo kwa kuongeza kifungu kipya cha 205A, kinachoainisha masharti kuhusu kupokelewa taarifa za wataalamu kama ushahidi mahakamani,” alisema.

Profesa Kabudi alisema katika sehemu ya tano ya muswada huo inapendekezwa kurekebishwa kwa tafsiri ya maneno ‘Katibu Mkuu’ kwa kumuondoa Naibu Mwanasheria Mkuu kwa kuwa katika muundo wa awali alikuwa Katibu wa Wizara lakini kwa sasa Naibu Mwanasheria ni msaidizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Sehemu ya Sita ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Ukomo Sura ya 89, kifungu cha 44, kinampatia waziri mwenye dhamana mamlaka ya kuongeza ukomo wa muda wa kufungua shauri mahakamani.

“Muswada unapendekeza kifungu hicho kirekebishwe kwa kuongeza masharti ambayo yatamwezesha waziri kutunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa mamlaka ya kuongeza muda wa kufungua mashauri ya madai nje ya muda.

“Pia muswada unapendekeza kurekebisha kifungu cha 11 kwa kuweka utaratibu mbadala wa kuchukua maelezo ya shahidi kwa njia ya kiapo bila kulazimika maelezo hayo kuchukuliwa mbele ya mahakimu kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 11 (2) cha sasa,” alisema.

Profesa Kabudi alisema, Serikali pia inapendekeza kuongeza vifungu vipya vya 38A, 38B, na 38C, kwa lengo la kupokea maelezo na uthibitisho wa nyaraka za viapo ambapo kwa sasa sheria haina masharti kuhusu namna ya kupokea maelezo na ushahidi wa nyaraka ambapo maelezo hayo yanaweza kutumika kama ushahidi katika mazingira ambayo shahidi aliye nje ya nchi hawezi kuja Tanzania kutoa ushahidi.

Aidha, wakitoa maoni yao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema utaratibu wa kutunga sheria na kufuatiwa na kanuni umekiukwa na serikali ya awamu ya tano ambayo imekuwa ikianza kutoa matamko na maelekezo kwanza ndipo utaratibu wa kisheria unafuata.

Pamoja na mambo mengine, alisema katika sehemu ya 13, inapendekezwa kurekebisha kifungu cha 38 kifungu kidogo cha (1) kwa kuweka masharti yatakayomwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwasilisha mahakamani maombi ya upande mmoja ya kukamata mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu na ambayo iko hatarini kupotea au kuharibiwa.

“Aidha, kifungu kidogo cha (6) kimeongezwa katika kifungu hicho ili kuiwezesha mahakama kutoa amri ya kutaifisha au kuuza mali iliypkamatwa na ambayo inaharibika upesi au ile ambayo utunzaji wake ni gharama kubwa,” alisema.

KAMBI RASMI YA UPINZANI
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF), alisema serikali imekuwa ikikiuka utaratibu wa utungwaji wa sheria kwa kuanza kutoa matamko na maelekezo na kisha unafuata utaratibu wa kisheria.

Alisema serikali hutakiwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, ibara ya 63 (3) (d) ya Katiba, inalipa bunge mamlaka ya kutunga sheria ambapo alihoji kama serikali inatoa maelekezo kupitia kwa rais au mawaziri na baada ya hapo kuleta muswada wa sheria kughalalisha maamuzi na maelekezo ya serikali ni ishara kuwa serikali inapuuza mamlaka na hadhi ya bunge.

“Mwaka 2016 akiwa katika mkutano mkuu wa CCM, Rais John Magufuli alitangaza na kuelekeza serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma bila uwepo wa sheria.

“Pamoja na Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ya Bunge kuhoji jambo hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa kauli kuwa jambo hilo linatakiwa kufanyiwa kazi na Ofisi ya Waziri Mkuu huku akijua yeye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali bila kujali wizara na idara,” alisema.

Akizungumzia marekebisho ya Sheria ya TLS, Saleh alisema sheria hiyo inawanyima haki watumishi wa umma, madiwani, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa kuwa wajumbe wa Baraza la Uongozi wa chama hicho.

“Mwanzoni mwa mwaka huu serikali iliingia mgogoro na TLS baada ya kuweka vifungu hivyo kwenye kanuni za uchaguzi bila kuzingatia kuwa hayakuwa ya Baraza la Uongozi na wala Mwanasheria wa Serikali hana mamlaka ya kufanya hivyo.

“Mawakili wanajua kuwa lengo la Ofisi ya Mwanasheria kuleta mapendekezo haya ilikuwa ni kumzuia Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki), kuendelea kugombea tena wadhifa wa urais wa chama hicho baada ya kuiona hawana namna ya kumzuia kwa njia nyingine yoyote au pengine wasiwasi juu ya umaarufu mkubwa aliojizolea Rais wa sasa wa TLS, Fatma Karume kwenye jamii wa kujiunga na siasa,” alisema.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuwa serikali inatunga sheria kwa kumlenga mtu au taasisi na haitungwi kwa malengo mahsusi ya kuwasaidia wananchi.

MAONI YA KAMATI
Aidha, akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Katiba na Sheria, Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro (CCM), alisema kamati imeshauriana na kukubaliana na seriklai kuyafanyia kazi kwa wakati mwafaka maoni ya kuhuisha sheria ya TLS.

“Sheria ya TLS imeanza kutumika nchini tangu Januari 1, mwaka 1955 na tangu wakati huo haijafanyiwa maboresho ya msingi kuhusu malengo, muundo na mfumo wa uendeshaji wake hali inayosababisha changamoto zinazoenekana sasa kwa chama hicho kushindwa kuendana na zama zilizopo.

“Kamati inaishauri serikali ifanyie tathmini sheria hiyo kwa kuzingatia masuala ya kubainisha na kutenganisha mamlaka na majukumu ya Baraza la TLS na sekretarieti yake, kuboresha masharti ya mkutano wa TLS, kuboresha masuala ya fedha ya TLS na kuweka masharti kuhus chapter za chama hicho,” alisema Dk. Ndumbaro.

MUSWADA WASHINDWA KUPITA
Hata hivyo, muswada huo ulishindwa kupita kutokana na akidi ya wabunge kutotimia hatua iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, kuahirisha shughuli hiyo hadi Jumatatu Septemba 10, mwaka huu.

Hatua hiyo ilikuja wakati Bunge lilipoketi kama kamati ili kupitia vifungu vya muswada huo na marekebisho yake na kisha kuupitisha baada ya Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, kuomba utaratibu kwa Mwenyekiti kuhusu akidi ya wabunge kabla ya muswada kupigiwa kura.

Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee

Mdee alisema kwa kutumia kanuni ya 88 (10) 77 (3) kuhusiana na akidi ya vikao vya bunge kwamba wanaenda kufanya maamuzi ya kupitisha muswada huo kifungu kwa kifungu na hatimaye kupitisha sheria lakini idadi ya wabunge wanaotakiwa kuipitisha ni wachache.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kutumia kanuni ya 88 (10) lakini vilevile na kanuni ya 77 kama ambavyo unaona, sasa hivi tunaingia kwenye kamati ya Bunge na tunaelekea kufanya maamuzi ya kupitisha kifungu kwa kifungu na hatimaye kupisha sheria hii kwa ajili ya mabadiliko haya ya sheria mbalimbali.

“Sasa mheshimiwa ndiyo kama vile unavyoona hapa, sihitaji kutumia nguvu nyingi sana kukushawishi hili bunge lina wabunge 393 na nusu ya akidi ni 193.

“Kwa makadirio ya chini lakini tunaoenda kufanya uamuzi tupo 67, tumeshajihesabu, kwa hiyo kwa sababu kanuni inaturuhusu kupiga kura kwa kengele basi tupige kwengele, tusubiri kama watu wapo nje basi waje na ikishindikana itabidi tuahirishe shughuli hii kwa leo,” alisema Mdee.

Mara baada ya Mdee, kusema hayo, Mwenyekiti wa Bunge alisema suala hilo litatolewa uamuzi wakati wa kupiga kura ambapo aliendelea kusoma vifungu vya sheria hiyo na mara baada ya kumaliza, Mdee alisimama tena kumkumbusha suala la akidi kutotimia.
“Sasa nilikuwa naomba kiti chako kwa kutumia kanuni ya 77 utoe maelekezo kengele ipigwe kwa dakika tatu ili waliokuwa nje waje, lakini pia utoe maelekezo kwa Makatibu wa Bunge watuhesabu ili kwa kumbukumbu za Bunge tujulikane wangapi kisha maelekezo ya kanuni yafuate,” alisema.

MANYANYA ATAKA WAKATWE POSHO
Baada ya Mdee kusema hayo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Injinia Stella Manyanya alitaka wabunge ambao wameondoka katika mkutano huo wakatwe posho za siku hiyo.

“Kwanza leo siku takatifu ya ibada kuna wengine wameenda kusali vile vile inawezekana kuna wale ambao wanakuwa ni wazembe wa kuhudhuria bungeni kwa hiyo endapo utaridhia kwamba itahesabika ikaonekana hatutoweza kutosha, ukiwatoa wale ambao wamekwenda msikitini, na walioomba udhuru basi wote wakatwe posho ya siku ya leo,” alisema.

Mwenyekiti wa Bunge aliamuru kupigwa kwa kengele ili kuita wabunge walioko nje na kusubiri kwa muda wa dakika tatu ambapo walijitokeza wachache lakini hata hivyo hawakutimia.

Kutokana na hali hiyo, Giga alisimama kuahirisha shughuli za bunge hadi Jumatatu.
“Dakika tatu zimeisha lakini naona kama wametimia au vipi? Waheshimiwa wabunge kwa vile kazi zote kwa siku hii ya leo tumezimaliza imebaki kulihoji bunge naahirisha shughuli zote za Bunge hadi saa tatu asubuhi,” alisema.

MAONI YA WABUNGE
Mara baada ya kuwasilisha muswada huo, baadhi ya wabunge walionesha kutokukubaliana na marekebisho hayo, huku baadhi yao wakidai kuwa marekebisho hayo yamewalenga baadhi ya watu.

MAKAMBA
Mbunge Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema), alisema suala la wanachama wa TLS wasiwe wanasiasa inakiuka katiba ya nchi ambayo inatoa fursa kwa kila mwananchi kugombea nafasi yoyote.

Alisema suala hilo linapaswa kuangaliwa kwa umakini kwani linawalenga watu fulani hapa nchini.

MTOLEA
Mbunge wa Jimbo la Temeke , Abdallah Mtolea (CUF) alihoja marekebisho ya vifungu vya TLS yanafanyika kwa lengo gani.

“Kwa nini hamleti marekebisho yote kwa pamoja? Mnadonoa donoa tu vifungu, mnaleta sheria kwa dhumuni la kuwakomoa watu, mnaleta marekebisho ili TLS iwe mkononi mwa Serikali, na mabadiliko haya ukiyasoma unapata picha ya Tundu Lissu na Fatma Karume,” alisema Mtolea.

Mbunge wa Jimbo la Temeke , Abdallah Mtolea

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles