25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

VURUGU ZAZUKA UGANDA, RAIA WATAKA JESHI LIMWACHIE BOBI WINE

KAMPALA, UGANDA           |             


MABOMU ya machozi na risasi moto yameikumba mitaa ya Kampala nchini hapa jana ahudhuri, baada ya askari polisi na wanajeshi kuwakabili waandamanaji waliowasha moto katikati ya barabara za Kisekka Sokoni, Namirembe na Soko la Kikuubo.

Vurugu hizo zimezua hofu ndani na nje ya mipaka ya taifa hili la Afrika Mashariki, huku baadhi, akiwamo Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), wakiitaka Serikali kuwaachia huru wabunge wa upinzani, ambao kukamatwa kwao ni chanzo cha machafuko hayo.

Kadhalika Serikali ya Uingereza imetoa taarifa ya tahadhari, ikiwaonya raia wake waliopo hapa au wanaotarajia kutembelea Uganda kuwa makini.

Umati ulikuwa ukiimba kaulimbiu ya Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ‘People Power. Our power’, wakitaka aachiwe huru.

Makumi ya watu walikamatwa katika operesheni hiyo iliyoendeshwa chini ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Dennis Namuwooza.

Waandamanaji wanaituhumu Serikali kuwatesa wabunge Bobi Wine, Francis Zaake na wengineo, wakiwamo wanahabari zaidi ya 30 waliokamatwa mjini Arua Jumatatu ya wiki iliyopita.

Walikamatwa baada ya kutokea vurugu baina ya wafuasi wa Mbunge mteule, Kassiano Wadri na wale wa mgombea wa Chama tawala cha NRM, Nusura Tiperu.

Vurugu hizo za Arua zilisababisha kifo cha dereva wa Bobi Wine, Yasin Kawuma na wengine wakipata majerahi ya risasi.

Aidha Jumapili mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na wengine watano kujeruhiwa baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakiendesha uasi katika Manispaa ya Mityana.

Vurugu hizo za juzi ziliibuka baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa Zaake amefariki dunia kwa kipigo kutoka kwa maofisa wa usalama anakoshikiliwa yeye na wenzake.

Kwa mujibu mmoja wa mashuhuda, Yunus Musa, aliyekufa alikuwa mmoja wa mashabiki wa soka kutoka Kaunti ya Singo waliokuwa wakielekea Kyaggwe, wilayani Mukono kutazama mechi.

Alisema polisi waliirushia risasi teksi waliyokuwa wakisafiria baada ya dereva kugoma kusimama. 

ZITTO ANENA

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini nchini Tanzania, amemtaka Rais Yoweri Museveni kumwachia huru Bob Wine na wabunge wengine mara moja.

Katika barua yake ya jana kwenda kwa Museveni, ambayo gazeti hili limeiona, Zitto alisema chama chake cha mrengo wa kushoto, kimekuwa kikifuatilia kwa karibu hali ya kisiasa inayoendelea Uganda na kuingiwa hofu juu ya kuzidi kubanwa kwa uwanja wa kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

”Tumepata mshtuko na huzuni kubwa kwa kukamatwa na tuhuma za kuteswa chini ya ulinzi wa polisi kwa Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Mheshimiwa Robert Kyagulanyi, ambaye alimuunga mkono mbunge mteule wa Arua, Kassiano Wadri wakati wa uchaguzi mdogo wa Arua.

“Pia tunafahamu kukamatwa kwa wabunge wengine wa upinzani akiwamo Mheshimiwa Gerlad Karuhanga, Mheshimiwa Paul Mwiru na Mhesdhimiwa Kassiano Wadri, ambaye pia anatuhumiwa uhaini kama ilivyo kwa Mh. Kyagulanyi,” Zitto aliandika katika barua hiyo.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, alimtaka Museveni kumwachia Bobi Wine na wenzake kwa vile hawajatenda kosa lolote na kumtaka aache kukandamiza viongozi wa upinzani.

“Kufuata misingi ya haki za binadamu, kunapaswa kuwa kipaumbele licha ya mtazamo wako kinzani kisiasa. Na kama kiongozi mwandamizi wa Afrika Mashariki, mwenye chembe ya mapinduzi, unatarajiwa kuonyesha viwango vya juu vya demokrasia na masuala ya heshima ya utu.

“NRM ni vuguvugu la ukombozi, halipaswi kuvumilia ukiukaji wa heshima ya utu iliyoonyeshwa na polisi na jeshi katika wiki za karibuni. Muhimu zaidi dhidi ya maofisa wa kuchaguliwa wa Uganda. Je, vijana wa Afrika Mashariki watajifunza nini kutoka kwa uongozi wako?” aliandika.

Aidha Zitto alimkumbusha Museveni namna Watanzania walivyomsaidia wakati wa harakati zake za kupambana na udikteta nchini Uganda, hivyo afute mashtaka yote dhidi ya Bobi Wine na wenzake na kumruhusu Wadri kuchukua kiti chake cha ubunge. 

MUSEVENI AKANA WINE KUWA MAHUTUTI

Hata hivyo, kuhusu utata wa hali za wabunge hao, Rais Museveni amekana hilo akivishutumu vyombo vya habari kwa kile alichosema kueneza habari zisizo na ukweli kuhusu suala hilo.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari, mbunge huyo ambaye pia ni msanii, ana matatizo ya figo yanayohitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea.

“Vyombo vya kueneza habari zisizo za kweli vimekuwa vikitangaza kuwa mjukuu wetu, asiye na nidhamu Bobi Wine, ni mgonjwa mahututi, hawezi kuzungumza na mengineyo.

“Wamekuwa wakisema kuwa huenda maofisa wa usalama wamemjeruhi vibaya Bobi Wine kwa sababu ya namna walivyokabiliana na wabunge wakati wakiwakamata.

“Nimeamua kuwasiliana na madaktari wa jeshi, kwa sababu ya nidhamu ya jeshi, madaktari wa jeshi daima wanachukua tahadhari katika hali kama hizi. Tayari Bobi Wine alionana na madaktari Arua, Gulu na Kampala. Hakuwa na majeraha ya kichwa, kifua au mifupa kuvunjika, wamenitaarifu,” ilisema taarifa ya rais.

Kadhalika Museveni alilaumu watu ambao alieleza kuwa ni wa nje wanaotafuta kuingilia siasa za nchi yake.

Hata hivyo, Chama cha Wafanyakazi wa Afya nchini Uganda, kimesema mahali wanapohifadhiwa wabunge wa upinzani na vyombo vya usalama akiwemo Bobi Wine mwenye matatizo ya figo, ni ya hatari na kunaweza kuwasababishia vifo.

Waganda walioko nje wameendelea kutuma ujumbe wa kuishutumu Serikali kwa vitendo vyake vya kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani na raia kwenye mitandao ya jamii.

UINGEREZA, EU ZAONYA

Aidha machafuko hayo yamekosolewa kote duniani, huku Umoja wa Ulaya ukisema yanachafua taswira ya Uganda.

Serikali ya Uingereza imetoa onyo kwa raia wake wanaosafiri Uganda kutokana na hali tete ya kisiasa.

Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola ikisema kuna uwezekano wa kutokea machafuko makubwa katika nchi hiyo kufuatia kukamatwa kwa wabunge kadhaa wa upinzani.

“Kuna uwezekano mkubwa wa maandamano makubwa, ambayo yategeuka machafuko kote nchini Uganda,” ilisema taarifa hiyo.

Katika mji wa Toronto, Canada, maandamano makubwa yalifanyika Jumamosi, huku raia wengine nao wakituma kanda binafsi za video kutoka Afrika Kusini na Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles