25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KURUSHA TELEVISHENI ZA NDANI MILIONI 900/-

PATRICIA KIMELEMETA NA LEONARD MANG’OHA – Dar es Salaam


KAMPUNI za visimbuzi za Azam, Dstv na Zuku, zitalazimika kulipa Dola za Marekani 400,000 sawa na takribani Sh milioni 913 ili kubadilishiwa aina ya leseni walizonazo kwa sasa.

Baada ya kubadilishiwa leseni, kampuni hizo zitasajiliwa nchini na kuweza kuonyesha vituo vya televisheni ambavyo kwa sasa wamevitoa kwenye visimbuzi vyao kutokana na agizo la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kwa sasa kampuni hizo zina leseni ya kuruhusu matangazo ya televisheni ya kibiashara.

Dk. Mwakyembe, alisema kwa sasa leseni ya kampuni hizo ni Dola za Marekani 100,000 sawa na Sh milioni 228.26.

Alisema wakati kampuni hizo zikitozwa kiasi hicho cha fedha, Star Media, Ting na Continental ambazo leseni zao zinaruhusu kurusha televisheni za ndani za bure, zinalipa Dola za Marekani 400,000 (Sh milioni 913).

Dk. Mwakyembe, alisema wizara yake inasimamia mahudhui, hivyo ni vema akalizungumzia suala hilo ili kuondoa sintofahamu iliyopo kwa wananchi.

Alizitaja chaneli zinazopaswa kuonyeshwa bure kwa wananchi ni TBC, Star TV, ITV, Channel Ten na EATV.

Dk. Mwakyembe, alisema kwa mujibu wa sheria, TBC lazima ionekane kwenye kila kisimbuzi kwa sababu ni mali ya Serikali.

Alisema kinachofanywa na kampuni hizo kwa sasa ni ukiukaji wa mikataba yao kwa kuonyesha chaneli hizo bila leseni, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

“Licha ya kutokuwa na leseni ya kuonyesha chaneli hizo, pia kampuni hizo zimekuwa zikiwatoza wananchi fedha ili kupata chaneli za ndani ambazo zinapaswa kuonyeshwa bure,” alisema.

Alisema ikiwa kampuni hizo zitahitaji kuonyesha chaneli hizo, zinapaswa kwenda TCRA ili zipewe utaratibu wa kupata leseni itakayoziwezesha kufanya kazi hiyo.

“Lakini kama hawa wenzetu wana hamu sana na soko hili la ndani, wasitumie njia za chini chini, badala yake waende TCRA wapewe utaratibu wa kufuata ili wapate leseni za kuonyesha chaneli za ndani, ikiwa watashindwa kufanya hivyo, wanapaswa kufuata utaratibu wa leseni zao,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema kampuni hizo zinaendesha shughuli zao kwa njia ya kidigitali, huku zikifuata lengo la kimataifa, ndiyo maana hata mitambo yao imesimikwa nje ya nchi.

Alitolea mfano wa kampuni hizo na nchi walizoweka mitambo kwenye mabano ni Azam TV (Mauritius), DSTV (Dubai) na Zuku ambayo mitambo yake imesimikwa nchini Kenya.

Aliongeza TCRA inaendelea kuzifuatilia kampuni hizo ili kuangalia kama wanafuata utaratibu huo na ikiwa watashindwa watachukulia hatua za kisheria.

Alisema hadi sasa kampuni zinazopaswa kurusha matangazo ni Star Media, Ting na Continental ambazo zililipa leseni ya Dola za Marekani 400,000 na kukidhi masharti ya urushaji wa matangazo hayo.

Dk. Mwakyembe, alisema miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kuwataka kuweka miundombinu ya mitambo yao ndani ya nchi, kupunguza gharama za visimbuzi ili chaneli za ndani ziweze kuonyeshwa bure na kurusha kwa kutumia satelaiti.

“Ikiwa kampuni hizo zitatoza fedha kwenye chaneli hizo, zitakuwa zimekiuka mkataba wa makubaliano yao, jambo ambalo litawafanya TCRA kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema.

Dk. Mwakyembe, alisema licha ya kujitokeza kwa mkanganyiko huo, lakini tayari Kampuni ya Star Media inayotumia kisimbuzi cha Startimes, tayari imeshatozwa faini ya Sh milioni 100, kutokana na kuwatoza wananchi fedha kwa kuona chaneli za ndani.

Alisema kutokana na hali hiyo, kampuni hiyo inaunga mkono kauli iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe ya kwamba ikiwa wataona sheria ina matatizo, wanapaswa kurudisha upya mchakato wa kutoa maoni hadi kufikisha bungeni kufanya marekebisho.

Dk. Mwakyembe, pia alisisitiza kuwa Serikali haijafuta leseni za visimbuzi vya Azam, Zuku na Multichoice Tanzania bali wanawataka kuondoa chaneli ambazo zinatakiwa kurushwa bure kulingana na matakwa ya mikataba yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles