27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MATAPELI WA KWENYE SIMU KIZIMBANI UHUJUMU WA UCHUMI

NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM


WATU 13 wanaodaiwa kutapeli watu fedha kwa ujumbe mfupi wa simu, wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka matano, yakiwamo ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha zaidi ya Sh milioni 154.

Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumain Kweka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nasoro Katuga.

Akisoma mashtaka, Wakili Katuga alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matano, ikiwamo kula njama, kuchapisha ujumbe usiofaa na mashtaka mawili ya kusambaza ujumbe huo na shtaka moja la utakatishaji wa fedha.

Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Boniface Maombe, David Luvanda, Moshi Sungura, Amos Bosco, Lule Kadenge, Jofrey Kapangamwaka, William Nturo, Regius Mauka, Collins Mwang’omolan, Francis Kapalata, Kasonde Kapela, Enock Mwandaji na Pascal Kiatu.

Katuga alidai shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Machi na Juni 2018, walitenda kosa la kula njama kwa kutuma ujumbe mfupi usiotakiwa katika maeneo ya Dar es Salaam, Rukwa na sehemu nyingine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia mfumo wa kumpyuta.

Katuga alidai katika kipindi cha Machi na Juni 2018, washtakiwa hao walichapisha taarifa za uongo zikiwa katika muundo wa ujumbe mfupi kupitia mfumo wa kompyuta kwa nia ya kudanganya.

“Shtaka la tatu ,washtakiwa wanadaiwa kusambaza ujumbe wa kielektroniki usiotakiwa kupitia mfumo wa kompyuta.

“Washtakiwa wote katika kipindi cha Machi na Juni 2018 katika maeneo ya Dar es Salaam na Rukwa, kwa njia ya kudanganya na kushawishi, walisambaza ujumbe mfupi wa kielektroniki kwenda kwa watu tofauti tofauti wakionyesha kuwa wanayo mamlaka ya kufanya hivyo wakati si kweli,” alidai Katuga.

Katika shtaka la nne, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho na maeneo hayo, kwa pamoja kwa nia ya kudanganya, walisambaza ujumbe mfupi usiofaa kwa njia za kielektroniki.

Katuga alidai washtakiwa wote katika shtaka la tano la utakatishaji wa fedha, wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho na maeneo ya Dar es Salaam, Rukwa na sehemu nyingine za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa moja walijihusisha na muamala wa Sh 154,032, 830 huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo hayo, hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo wala kutoa dhamana hadi Mahakama Kuu.

Shtaka la utakatishaji wa fedha ni miongoni kwa mashtaka yasiyo na dhamana.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Agosti 21, mwaka huu. Washtakiwa wamepelekwa rumande.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles