25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO: ABSALOM KIBANDA AMTUMIA UJUMBE RAIS JPM

Absalom Kibanda

NA ABSALOM KIBANDA, +255 782 377 070                       |                                 


HUU ni mwezi wa 21 tangu Serikali ya Rais wa tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli ishike hatamu ya kuiongoza Tanzania kwa namna ambayo ni rahisi kwa wachambuzi wa masuala ya uongozi kuufananisha na kisu kinachokata kuwili’.

Ningekuwa naiandika makala hii kwa lugha ya Kiingereza, ingetosha kuandika nikiuelezea uongozi wa Rais Magufuli kwa maneno haya; ‘Its no longer business as usual in Tanzania’ kwa tafsiri rahisi; ‘

Ninapata shida kukubaliana na ushauri au maelekezo yaliyotolewa na Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa alioutoa mbele ya JPM na viongozi wengine wakuu na wajuu wastaafu, wakati wa kikao chao kisicho cha kawaida kilichofanyika Ikulu Dar es Salaam hivi karibuni.

Klipu (clip) fupi iliyosambazwa na Ikulu saa chache baada ya kikao hicho cha Rais na viongozi hao wastaafu, ilimwonyesha Mkapa akiwataka viongozi wa sasa kuitambulisha Serikali ya Magufuli kuwa ni Serikali ya CCM.

Ni kweli, serikali inayoongozwa na Dk. Magufuli inatokana na CCM. Ni kweli pia kwamba hii ni Serikali ya Magufuli na hata CCM ya leo ni CCM inayoongozwa na Magufuli na kimsingi ni CCM ya Magufuli.

Nimelazimika kurejea kauli ya Mkapa kwa sababu mahususi. Kauli yake ilinirejesha na kunikumbusha safari ya kisiasa ya Rais Magufuli kutwaa mamlaka ya juu ya dola miaka mitatu iliyopita.

Alikuwa ni Magufuli mwenyewe ambaye katika majukwaa ya kampeni alikuwa bayana kuwashawishi wapigakura na kuwaandaa kwa kuwaambia iwapo atashinda ‘Serikali ya Magufuli’ itafanya hiki au kile kwa masilahi mapana ya taifa.

Matamshi hayo ya Dk. Magufuli, katika kipindi cha miezi 20 tangu aingie madarakani yamekuwa ndiyo mazungumzo ya majukwaani na ya ndani ya vikao miongoni mwa watumishi wa umma na wateule takribani wote wa kisiasa, ambao naamini maneno yao ndiyo hasa msingi wa kauli ya Mkapa.

Kwa muktadha wa makala hii, nina kila sababu ya kuungana na wale wanaoitambulisha Serikali ya awamu hii kwa jina la Serikali ya Magufuli, ambayo imebeba ajenda nyingi tofauti ambazo leo hii mashabiki wake wanazitanabahisha na kaulimbiu za ‘Tanzania Mpya’ ‘CCM Mpya’ ‘Dar es Salaam Mpya’ na nyingi zinazofungamanishwa na msamiati huo huo ‘mpya’.

Ni rahisi kufikia hitimisho la kuuona upya unaozungumzwa na kutendwa nyakati hizi za Magufuli, japo kwa msamiati tu kuturejesha kifikra na kutukumbusha zama zilizojaa mbwembwe nyingi za ‘Ari ‘Mpya’, Nguvu ‘Mpya’ na Kasi ‘Mpya’ nyakati za urais wa Dk. Jakaya Kikwete.

Ninao uhakika kwamba iwapo leo hii tutajiuliza ni upya gani wa msingi au wa maana ambao Tanzania iliuona nyakati zile za Kikwete, ni watu wachache ambao watakuwa na majibu bayana ya kuusemea na kutuonyesha matokeo ya fikra, nguvu na kasi zilizobebeshwa upya kwa kipindi chote cha miaka 10 cha kati ya mwaka 2005 na 2015.

Ninaweza nikaandika kwa kujiamini kwamba kaulimbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, ambayo Kikwete aliingia nayo madarakani kwa kishindo cha asilimia 80 ya kura zote mwaka 2005, ilihitimishwa vibaya na pengine kufa kabisa hata kabla ya muhula wake haujaisha.

Bado ninaweza nikazikumbuka vyema kauli za mawaziri wa nyakati za Kikwete, wakuu wake wa mikoa na wilaya, ambao walipita katika majukwaa mbalimbali ya kisiasa na wakati mwingine hata ya kikazi kama ndani ya Bunge ambako kaulimbiu hizo zilirejewa kwa mbwembwe nyingi.

Ilimchukua Rais Kikwete na Serikali yake miaka mitano tu ya kwanza ya utawala wake kubaini kwamba ule upya uliofinyangwa katika ari, nguvu na kasi uliishia katika viunga vya kisiasa na majukwaani na si katika mioyo ya Watanzania wapigakura.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimpokonya kura nyingi Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005, ni ushahidi wa kwanza wa namna upya ulivyoshindwa kutafsirika katika akili na pengine maisha halisi ya Watanzania.

Kilichotokea miaka mitano baadaye, yaani 2015 ndani ya CCM na namna mahasimu wa kisiasa wa Kikwete na Serikali yake walivyogeuka na kuwa watu wenye ushawishi mkubwa kisiasa, ni ushahidi mwingine wa kukwama au kutotafsirika vyema kwa upya uliobeba matumaini makubwa kwa Watanzania miaka 10 ya uongozi wake. Pengine kauli iliyopata kutolewa hadharani na mwanasiasa kijana, mtata ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, kwamba alishiriki katika kuitoa CCM shimoni wakati akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho (2012-2016), inatosha kukamilisha rejea ya mkwamo wa fikra za ‘upya’ wa zama za JK.

Waswahili wana msemo unaosema mwenzako akinyolewa wewe unatia maji. CCM ya Magufuli inapaswa kujifunza kutokana na makosa ya CCM ya Kikwete ambayo Nape na pengine makada wenzake wenye mawazo kama yake wanaamini waliitoa shimoni. Kama ilivyo kwa CCM, ndivyo inavyopaswa pia kuwa kwa Serikali ya JPM. Inapaswa kujifunza kutokana na makosa ya kauli, kimaamuzi na kimatendo ambayo yaliwagharimu mwaka 2010 na 2015.

CCM na Serikali yake watakuwa wanafanya makosa iwapo wataendelea kuamini kwamba kaulimbiu za Tanzania Mpya na CCM Mpya vinatosha kuwaaminisha mamilioni ya Watanzania wanaopiga kura, ambao idadi yao inaongezeka kila baada ya miaka mitano.

Upya wa Tanzania au CCM unapaswa kujengwa katika misingi madhubuti ya uongozi madhubuti na unaojali maisha na masilahi mapana ya watu milioni 55 wenye uhitaji mpana unaobebwa katika nadharia ya kiimani inayosema ‘mtu haishi kwa mkate tu’.

Upya wa Tanzania na wa CCM unapaswa kujengwa katika misingi ya kufufua na kuimarisha vilivyokufa, vilivyokuwa dhaifu au vile ambavyo vilikuwa imara na vinavyopaswa kuwekewa mizizi madhubuti.

Ni mpuuzi peke yake ambaye anaweza akasimama leo na akapuuza jitihada kubwa za Serikali hii za kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa namna ya kununua ndege mpya za kisasa kama Boeing 787-8 Dreamliner na Bombardier.

Rais John Magufuli

Ni mtu anayesahau majanga ya kihistoria ya sekta ya nishati ya tangu zama za mizozo kama ile ya kukauka kwa mabwawa ya Mtera na Kidatu, makaa ya mawe ya Kiwira, IPTL ya miaka ya mwisho ya 1990, Songas, Richmond na Dowans, anayeweza akaishia kuing’ong’a Serikali na Rais JPM badala ya kutoa ushauri unaopaswa ili mradi mkubwa wa Stiegler’s Gorge uweze kuanza.

Hata hivyo, tutakuwa tunafanya makosa makubwa iwapo tutakaa kimya wakati tukiona dhahiri namna Serikali inavyochukua uamuzi wa kuvuruga hata yale mazuri machache ambayo yalipaswa kuwa kioo cha mafanikio ya taifa hili yaliyofanywa wakati wa awamu zilizopita.

Upya wa Tanzania na CCM unaopigiwa chapuo, hauwezi ukawa na tija iwapo tutakaa kimya wakati tukishuhudia kuzorota kwa mzunguko wa fedha, ambao unatishia uhai wa biashara na uwekezaji wa ndani na nje kwa kiwango cha kuyumbisha au kuyaua mabenki, mahoteli, sekta za madini, hifadhi ya jamii, ujasiriamali na uwekezaji wa mitaji.

Ni mwendawazimu peke yake ambaye anaweza akapuuza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuifufua sekta ya utalii kwa namna tofauti ikiwamo hiyo ya kuifufua ATCL. Sisi pia tutakuwa ni wendawazimu iwapo tutakaa kimya pasipo kuhoji juu ya kuwapo kwa taarifa za kuzorota kwa biashara za hoteli, kudumaa kwa sekta ya benki na wasiwasi mkubwa uliotanda katika sekta ya hifadhi ya jamii.

Baadhi yetu bado tunajiuliza ulipoishia ule mzozo wa kiuwekezaji kati yetu na kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Acacia ambao ulilipaisha sana jina ‘makinikia’.

Wakati tukikubaliana kwa asilimia 100 na hatua ya Serikali kushtukia utaratibu ambao umekuwa ukiibua maswali mengi juu ya kusafirishwa nje ya nchi kwa mchanga wa dhahabu, tuna kila sababu pia ya kuwasikiliza wadau wengine mbalimbali ambao nao mchango wao kuhusu uimara wa sekta ya madini umekuwa ni kilio chao cha miaka mingi.

Dhamira zinatusuta sisi tulio katika vyombo vya habari ambao tumejipa dhamana na jukumu la kuwapasha habari Watanzania, tunaposhindwa kuwa na majibu juu ya mahali yaliko yale makontena yaliyozuiwa kusafirishwa nje ya nchi baada ya kufikishwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Wakati tukitii mamlaka na tukilazimika kuwaamini viongozi wetu wa Serikali na hususani Rais, kwamba mazungumzo kati ya Kampuni ya Barrick ambayo ndiyo mbia mkuu wa Acacia yanakwenda vizuri, bado tunao wajibu wa kujua iwapo kinachoendelea sasa si kile ambacho kiliwashinda watangulizi wa Magufuli.

Ni katika muktadha huo huo, upya wa Tanzania na CCM hautakuwa na maana iwapo tutaanza sasa kujenga taifa linalokaa kimya wakati watu wakiwa na shaka kwamba kuna kuzorota kwa mfumo wa demokrasia, kuwekwa kando kwa misingi ya utawala wa sheria, uongozi bora, uhuru wa mawazo, ule wa kutoa maoni na uhuru wa habari.

Hata katika haya pia, wakati tukiwa na wajibu wa kuwaelimisha wanasiasa na wananchi kwamba siasa za harakati na kampeni hazipaswi kufanywa ajenda wakati usio wake, Serikali na mamlaka zinapaswa kukumbushwa kwamba mkono wa chuma hauwezi ukawa na majibu yote ya kuliondoa taifa katika mwelekeo huo usiofaa.

Hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kuondokana na uholela katika siasa na demokrasia, zinapaswa pia kuendelezwa katika uhuru wa watu kutoa maoni yao pasipo kuvunja sheria, sambamba na kuviacha vyombo vya habari vikitekeleza wajibu wake kitaaluma na kwa kuzingatia maadili na miiko ya Kitanzania pasipo kumhofia yeyote.

Katika hilo pia, sisi ambao tunalifahamu hili, tunapaswa kutumia kila mbinu na njia zinazofaa na pasipo kuchoka kunyosha vidole na ikibidi kukemea pale tunapoona misingi mama ya utaifa wetu inakiukwa.

Nayaandika hayo nikiamini kwa dhati kwamba upya wa Tanzania na CCM hauwezi kuja kwa kubomoa misingi imara ambayo iliwekwa pamoja na makosa yote ya kiuongozi ya zama za Kikwete, Mkapa, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Nina kila sababu ya kuamini kwamba jemedari wa zama hizi, Rais Magufuli, atakubaliana nami iwapo nitaandika, tutakuwa tukifanya makosa makubwa iwapo tutaingia katika mtego kushabikia mtikisiko kwenye misingi ya utaifa wetu. Kufanya hivyo utakuwa ni mwanzo wa mkwamo. Hatupaswi na hatuna sababu ya kuanza upya.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. ni kweli yapo mambo mazuri aliyofanya magufuli lakini demokrasia inaminywa sana hivyo ni vema suala hili likawekwa wazi kwanini katika karne hii ambapo uwazi unatakiwa zaidi pia mzunguko wa hela unasuasua sanaa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles