Na PENDO FUNDISHA-MBEYA |
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, amekiri kuwa na matarajio ya kugombea nafasi ya ubunge katika moja ya majimbo ya Mkoa wa Mbeya.
Ingawa hakutaja jimbo ambalo atagombea, watu ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wake wanasema huenda akagombea Jimbo la Mbeya Mjini linaloongozwa na Mbunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi (Sugu) au Jimbo la Rungwe linaloongozwa na Sauli Amon wa CCM kutokana na miradi mingi inayotekelezwa na taasisi yake inayofahamika kama Tulia Trust kuelekezwa katika maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vilivyopo nyumbani kwake eneo la uzunguni jijini hapa, Naibu Spika huyo alisema ingawa anatambua ya kwamba dhamana ya uwakilishi ipo mikononi mwa wananchi, lakini ndani ya chama chake upo utaratibu hivyo wakati utakapofika ataamua.
“Wengi wamekuwa wakihoji kwamba je, nina nia ya kugombea? Na hata hapa kuna baadhi yenu mmeniuliza, ngoja niondoe sintofahamu hii, ni kweli nia yangu ya kugombea ubunge ipo lakini bado sijajua nitagombea wapi,” alisema.
Alisema CCM imeweka utaratibu mzuri kwa wanachama wake wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali na wale wanaotaka kuwawakilisha wananchi bungeni, hivyo haitakuwa busara kwake kuvunja kanuni, taratibu na sheria za chama.
Alisema kwa sasa anatekeleza majukumu ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Mbeya na nchi kwa ujumla wanapata maendeleo.
Kuhusu taasisi yake ya Tulia Trust, alisema imejipanga vema kuleta ukombozi wa Mtanzania kupitia sekta ya elimu.
Aidha, akizungumzia siasa zinavyokwamisha maendeleo ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Tulia aliwaasa watendaji na wanasiasa kuondoa siasa kwenye masuala muhimu ya maendeleo na kwamba atahakikisha anawasilisha changamoto hizo kwenye vyombo husika ili hatua kwa wahusika zichukuliwe.
“Waandishi mmeeleza mengi lakini kubwa ninaloliona ni changamoto za siasa kuingizwa kwenye utendaji kazi hasa kwenye mambo muhimu ya maendeleo, hili nitalifanyia kazi na kuangalia uwezekano wa kulikomesha kwani Mbeya itajengwa na Wanambeya wenyewe,” alisema.