28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TASAF YABISHA HODI WILAYANI MASASI

NA MWANDISHI WETU


JUMLA ya wajasiriamali 159 kutoka vikundi mbalimbali wilayani Masasi wanatarajiwa kufadika na miradi ya ufugaji wa samaki iliyofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).

Hatua hiyo imekuja kupitia miradi saba ya ufugaji wa sato waliyoibua kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini uliopo chini ya mfuko huo, ambapo itawasaidia kupata kitoweo na fursa ya kibiashara.

Akizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea miradi hiyo jana kiongozi wa kundi la walengwa hao wa Mtaa wa Madeko katika Halmashauri ya Mji wa Masasi, Hamidu Kindamba, alisema waliibua mradi huo baada ya kuona uwepo wa fursa ya mahitaji ya samaki hao wanaotoka Mwanza.

Alisema kilo moja ya samaki inauzwa Sh 10,000 hivyo watakavyoanza uzalishaji watapata kitoweo kwa bei nafuu ya Sh 8,000 na pia watakuwa na uhakika wa soko kwa wananchi wa maeneo mbalimbali.

“Katika bwawa letu tulilochimba kwa nguvu zetu kwa ufadhili wa TASAF, tumefuga sato 1,203 ambao sasa wana miezi miwili na tunatarajia kuvuna watakapofikisha miezi sita,” alisema.

Akizungumzia mradi huo mjasiriamali mwingine, Consolota Steven, alisema wananchi wa mji wa Masasi wanategemea samaki wa maji chumvi na baridi, ambapo kaya masikini zinakosa kula samaki kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na bei kubwa.

Mkazi wa Kijiji cha Nangose katika halmashauri hiyo, Beatus Mapeta, aliishukuru TASAF kwa utekelezaji wa mpango huo wa kunusuru kaya masikini.

Alisema kupitia ruzuku ya Sh 28,000 ameweza kuzitumia fedha hizo kuongeza uzalishaji wa korosho na mahindi na sasa kipato chake kinafikia Sh milioni mbili kwa mwaka.

Mapeta ambaye ana familia ya watu sita alisema fedha za hizo huzitumia kununua pembejeo na kuweka vibarua na hivyo kuwa na uhakika wa chakula na kusomesha kijana wake ambaye amemaliza kidato cha sita na sasa anasubiri kujiunga Chuo Kikuu.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Masasi, Jorum Msiyangi, alisema mabwawa saba yalichimbwa na kwamba baada ya mavuno ya awali fedha zitakazopatikana zitagawanywa kwa vikundi hivyo.

Alisema walengwa hao huwezeshwa na wataalamu kutoka halmshauri kuhusu ufugaji bora wa samaki, ikiwamo namna sahihi ya kuwapatia chakula. “Katika kila bwawa wameweka vifaranga 100 vinavyozaliana ili kupata mbegu baadae,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles