26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UKISIKIA STORI ZA LAVA LAVA UTAZIPENDA!

Na CHRISTOPHER MSEKENA

MIONGONI mwa vijana wapya wanaofanya vyema kwenye muziki wa Bongo Fleva kwa sasa ni Abdul Iddi ‘Lava Lava’, msanii kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby  (WCB) inayomiliki wasanii wengine kama Rayvanny, Harmonize, Queen Darleen na Diamond Platnumz ambaye ndiye bosi wa lebo hiyo.

Kutoka Sinza Kijiweni mpaka karibu na hoteli moja yenye hadhi ya nyota 3 iliyopo hatua kadhaa mbele ya Mlimani City, Dar es Salaam zilitumika dakika zisizozidi 15 kulifikia eneo hilo tulilopanga kukutana na Lava Lava kwa ajili ya mazungumzo yetu.

Nilipofika nikakaribishwa na mwenyeji wangu, tukavuta viti, kinywaji changu kilikuwa ni maji na yeye nilimkuta anakunywa  taratibu soda na tukaanza mazungumzo yetu.

AJENGA JINA MTAANI

Anasema safari yake ya muziki ilianzia mtaani kwao, Bunju ambapo alijenga jina lake kwa kuimba nyimbo za watu kiasi asipokuwepo mtaani hapo pengo lake huonekana.

“Nilikuwa mtu fulani wa kupiga sana kelele mtaani, majirani sasa wakawa wananiambia kwanini nisiende kujiunga na mashindano ya Bongo Star Search, nikawa napuuza, nacheka naachana nao, nikawa hivyo mpaka shuleni.

“Kuna siku mtaani kulikuwa na Mzee John, mkali sana, alinikuta ninaimba akapita, akarudi tena nyuma na kuniuliza kama ni mimi nilikuwa naimba, nikamwambia ni mimi akanisifia nina kipaji sana, nikaanza kutambua nina kitu ndani yangu,” anasema.

ATOROKA SHULE, ATUA THT

Ilifika kipindi muziki ulimtawala zaidi kuliko masomo, akaanza kutoroka ili apate muda wa kwenye nyumba ya vipaji (THT).

“Nikawa nikienda shule naweka nguo za nyumbani kwenye begi, nikitoka shule naenda THT kuimba, jioni napitia tena kwa rafiki yangu Mwenge navaa sare za shule narudi tena nyumbani,” anasema.

ATUNUKIWA CHETI

Lava Lava anasema baada ya kupita kwenye mchujo wa wasanii wachanga zaidi ya elfu moja na kuingia 50 bora, alifanya mafunzo ya muziki THT kwa miaka mitano na kukabidhiwa cheti cha masuala ya muziki na kupewa ruhusa ya kuingia mtaani kusaka menejimenti.

MCHONGO WALETWA

Anasema kuna rafiki yake ambaye alikuwa ni dansa, alimtonya kuwa pale WCB kuna nafasi imetokea ndipo alipofanya michakato ya kuipata nafasi hiyo na kukutana na jamaa baunsa lenye madevu linaloitwa Mafia ambaye alikuwa kiongozi anayeogopwa zaidi pale WCB.

URAFIKI NA MAFIA, LAIZER

Anasema: “Nilitengeneza urafiki na Mafia ili nipate nafasi za upendeleo na baadaye nikawa karibu na prodyuza Laizer, kipindi hicho na yeye anatafuta nafasi, nikawa namwambia Diamond akiwa karibu na studio basi acheze nyimbo zangu ili Simba azisikie.”

MWAKA BILA KUMWONA DIAMOND

Anasema alikaa mwaka mzima kwenye ofisi za WCB bila kuonana na Diamond licha ya kwenda kila siku katika ofisi hiyo.

“Mafia alikuwa ananificha kila Diamond akiingia ofisini kwa hiyo nilikaa mwaka mzima bila kukutana naye kumbe alikuwa anasikia nyimbo zangu lakini hanionyeshi kama ananikubali,” anasema.

KAVA YAMPA KIBALI

Lava Lava anasema baada ya kuurudia wimbo wa ‘Utanipenda’ ulioimbwa na Diamond Platnumz na kufanya video ndipo milango ilipofunguka kwani alisifiwa live na Chibu mwenyewe.

Jambo hilo lilisababisha mshkaji wake Lukamba aliyetengeneza video hiyo apate dili WCB kama mpiga picha jongevu (video) wa Diamond Platumz.

AJARIBIWA TENA

Moja ya jaribu jingine alilopewa ni pale ambapo Diamond Platnumz alitaka anunue wimbo wake ili autumie yeye..

“Mimi nikamwambia achukue bure, akanibadilikia akaniambia simfai sababu yeye anataka wafanyabiashara kwani hata Zari alimlipa, mama yake mzazi alimlipa na pia Tiffah alimwingizia fedha yake benki waliposhiriki kwenye video ya Utanipenda.

“Ikabidi nimwambie milioni 3, akaniambia poa nitakuona. Ule wimbo mpaka leo upo studio, hajaununua kama ikitokea atauchukua atanipa hela, ndiyo nikaanza kurekodi nyimbo na mwezi wa saba nikatolewa rasmi,” anasema Lava Lava.

PICHA TATU ZA DIAMOND

Lava Lava anasema hana jambo lolote la kumshauri Diamond kwa sababu msanii huyo ana maisha ya aina tatu ambayo yote anaishi sawa.

“Kitu ambacho wengi hawajui kwa Diamond ni kwamba ana picha kama tatu anazoishi nazo kwenye mwonekano wake, kuna maisha ya nje ambayo wengi wanayajua nyinyi waandishi na mashabiki.

“Kuna maisha ambayo anaishi na sisi wafanyakazi wake kama marafiki na washkaji zake na kuna yale anayoishi na wazazi wake. Diamond yupo sawasawa kila engo anayoishi,” anasema.

TOP  5 YA WAREMBO

Lava Lava amewataja warembo Tunda, Naj, Wema Sepetu, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya na Lulu ni miongoni mwa warembo wakali watano kutoka sanaa mbalimbali Bongo anaowakubali zaidi.

Alipotakiwa kueleza sababu za kuvutiwa na madiva hao, alijibu kifupi kuwa: “Kazi zao ni nzuri. Napenda wanavyojituma.”

USHIRIKINA KWENYE VIDEO

Ndani ya Januari, tayari ametoa nyimbo tatu ambazo ni Teja, Kilio na Utatulia lakini kuna changamoto ambayo hawezi kusahau wakati wa uchukuaji picha za video ya Kilio iliyofanyika kwenye kijiji kimoja nje ya Dar.

“Tulikwenda watu zaidi ya 80, changamoto ilikuja baada ya kuanza kuhisi kuna mambo ya Kiswahili, giza linaingia na majenereta yakaanza kuzima.

“Baadhi yetu wakapandisha mashetani jambo lililofanya tuondoke kwenye baadhi ya maeneo kwenye kijiji hicho kwa kufuata utaratibu tuliopewa na wale waliopandisha mashetani.

“Ni tukio la ajabu lililosababishwa na kutokuelewana na wenyeji tuliokuwa tukishirikiana nao kwenye utayarishaji wa video hiyo. Ilibidi tuondoke haraka usiku huohuo…aisee uchawi upo,” anasema Lava Lava.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles