Na LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amezindua Mwongozo wa Matibabu na orodha ya dawa muhimu za taifa, utakaotumiwa kutibu magonjwa mbalimbali nchini.
Mwongozo huo utaweka utaratibu maalumu wa uandishi na uagizaji wa dawa kwa ukizingatia ngazi ya hospitali husika.
Pia utaonyesha aina gani ya dawa itumike katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya, mkoa na rufaa na kuzuia wahudumu wa afya kutoa dawa kwa wagonjwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi kupitia kampeni ya ‘Tuimarishe Afya”, Waziri Ummy alipiga marufuku wakurugenzi wote kuagiza dawa zisizo katika mwongozo huo.
“Upatikanaji wa dawa ni muhimu kwa kila mtu, sasa changamoto ya ukosefu wa dawa tulionao unasababishwa na matumizi mabaya ya miongozo ya Serikali.
“Tunapokwenda Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) tunakuta dawa zipo, lakini ukienda kutembelea hospitali wananchi wanalalamika kuwa wanaandikiwa dawa ambazo hazipo, tulichogundua wataalamu wetu wa afya huwaandikia wagonjwa dawa zisizo kwenye mwongozo ili waende wakanunue kwenye maduka yao, tena kwa bei kubwa,” alisema Waziri Ummy.
Alisema mwongozo huo utaruhusu baadhi ya dawa ambazo hazitolewi katika vituo vya afya na zahanati, zikiwamo dawa za kisukari na za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) kuanza kutolewa.
Kuhusu udhibiti wa usugu wa dawa unaosababishwa na matumizi holela ya antibiotiki, Waziri Ummy alisema wamezigawanya dawa hizo katika makundi matatu kulingana na hadhi ya hospitali.
“Kundi la kwanza litatambuliwa kwa jina la Access ambazo zitapatikana katika zahanati na vituo vya afya vyote, Watch zitatolewa na hospitali za wilaya na mikoa, na kundi la mwisho ni Reserve ambazo zitatolewa na hospitali za kanda, rufaa na maalumu za kitaifa.
“Ninasema antibiotiki ya kundi la Reserve haitapatikina katika ngazi ya zahanati na kituo cha afya, nitashangaa mkurugenzi atakayeomba dawa ya hospitali ya rufaa azipeleke zahanati,” alisema Waziri Ummy.
Aliutaka Mfuko wa Afya wa Taifa (NHIF) kuandaa orodha ya dawa zitakazotolewa kwa wanachama wao kwa kuzingatia mwongozo huo.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari, alisema mwongozo huo umeandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili uguse maeneo yote muhimu na kwamba anategemea wahudumu wa afya kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa itakapojitokeza changamoto ya utumiaji wa mwongozo huo.