27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA ATOBOA SIRI MAZUNGUMZO NA MAGUFULI

Na ASHA BANI – DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ameeleza alichozungumza na Rais Dk. John Magufuli, walipokutana Ikulu Dar es Salaam wiki iliyopita.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema Rais Magufuli alimshawishi arudi CCM, lakini alimkatalia kwa kuwa uamuzi wake wa kukihama chama hicho haukuwa wa kubahatisha.

Kutokana na hali hiyo, Lowassa amewatoa hofu Watanzania na kuwahakikishia kwamba hayumbi na hayumbishwi na kuwa yuko imara kuliko wakati mwingine wowote.

“Mnamo Januari 9 mwaka huu, nilipokea mwaliko kutoka kwa Rais Dk. John Magufuli akiniomba kwenda kukutana naye Ikulu siku hiyo hiyo kwa ajili ya mazungumzo.

“Aidha, Jumapili ya Januari 14, 2018, nilipata fursa ya kukieleza kwa kina chama changu kupitia kikao cha Kamati Kuu juu ya mazungumzo yangu na Rais Dk. Magufuli Ikulu.

“Ujumbe wa Rais Dk. Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwangu, ilikuwa ni kunishawishi kutaka nirejee CCM, suala ambalo sikukubaliana nalo.

“Nilimweleza Rais, kwamba uamuzi wangu wa kukihama CCM na kujiunga na Chadema haukuwa wa kubahatisha.

“Kwa hiyo, baada ya ujumbe huo wa Rais Dk. Magufuli, nilitumia fursa hiyo kujadiliana na Rais juu ya masuala mbalimbali ya msingi kuhusu nchi yetu.

“Masuala hayo ni kuhusu kutoheshimiwa kwa katiba na sheria, uminywaji wa demokrasia, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaohusisha kupotea kwa watu, kuvamiwa, kutishwa na kushambuliwa kwa viongozi wa kisiasa wa upinzani na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi wetu.

“Ni imani yangu, kwamba Rais atayazingatia na kuyafanyia kazi masuala haya kwa masilahi ya nchi yetu.

“Kupitia taarifa yangu hii, nawajulisha Watanzania wote wapenda mabadiliko ya kweli, kwamba nipo imara na madhubuti kuliko wakati mwingine wowote ule.

“Sijayumba na wala sitoyumba, ninaendelea na dhamira yangu ya kuamini katika Chadema na kusimamia mabadiliko kupitia Ukawa,” alisema Lowassa kupitia taarifa yake hiyo.

Januari 9, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Ikulu Dar es Salaam.

Kikao hicho cha dakika 45 kilifanyika jana huku wawili hao wakielezana yaliyo ndani ya mioyo yao.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa baada ya mazungumzo hayo, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.

Msigwa alisema kuwa Lowassa aliyataja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo na ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Mbali na hayo, alitaja pia ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mheshimiwa Rais (John Magufuli), tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo.

“Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo,” alisema Lowassa.

Alisema lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, elimu, kwani ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya.

“Hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mheshimiwa Rais (John Magufuli), you made my day,” alisema Lowassa.

Kwa upande wake, Rais Magufuli, alimpongeza Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali na huku akimwelezea kuwa ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake ametoa mchango wake katika nchi.

“Mheshimiwa Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo (jana) nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Mheshimiwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri.

“Na mimi napenda kumpongeza Mheshimiwa  Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.

Hata hivyo, dakika chache baadaye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisikika akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW), akionyesha kutoridhishwa na kauli za Lowassa juu ya Serikali iliyoko madarakani.

Mbowe alisema kilichoelezwa na Lowassa, ulikuwa ni msimamo wake binafsi wala haukuwa msimamo wa Chadema.

Pamoja na Mbowe, baadhi ya wanachama wa Chadema akiwamo Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), walilaani pongezi za Lowassa dhidi ya Serikali kwa kuwa hawaridhishwi na mwenendo wa masuala mbalimbali nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles