25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MSHTUKO VIFO VYA WATOTO MUHIMBILI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


IDADI kubwa ya watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda (njiti) wanahofiwa kufariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kukosa hewa ya oksijeni.

Hewa hiyo ilikuwa ikiwasaidia kupumua baada ya umeme kukatika ghafla.

Taarifa zilizopatikana hospitalini hapo zinaeleza kuwa upungufu wa hewa hiyo muhimu kwa vichanga hao  ulitokana na kukatika umeme hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo hospitalini hapo, baada ya umeme kukatika iliwashwa jenereta lakini haikuwa na nguvu ya kusukuma oksijeni na kusababisha vifo hivyo.

Mmoja wa ndugu wa mzazi aliyepoteza mtoto katika tukio hilo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini, alisema Januari 12 mwaka huu, mdogo wake alimwarifu kwamba mkewe alikuwa amefanyiwa upasuaji Muhimbili na kubahatika kupata mtoto wa kiume.

Alisema kwa kuwa mtoto alikuwa hajatimiza muda wake, alilazimika kuwekwa katika chumba cha watoto ‘premature’ na kwamba hali yake ilikuwa nzuri hadi Januari 13.

“Siku hiyo ya Januari 13 saa 4.00 wakati mtoto alipokuwa akilishwa chakula, ghafla umeme ulikatika. Waliwasha jenereta, lakini pamoja na kuwaka mara moja hali ya mtoto ilibadilika ghafla na hatimaye kupoteza uhai.

“Mdogo wangu alimzika mwanawe katika makaburi ya Tambaza jana (juzi) jioni ambako vichanga wengine watatu walizikwa miongoni mwa waliopoteza maisha hapo Muhimbili,” alisema.

Mzazi mwingine aliyefiwa na mwanawe aliiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina kujua ukweli kuhusu vifo hivyo.

“Mke wangu alisema alishuhudia mtoto akipoteza maisha na wengi walifariki dunia kwa sababu ya uzembe wa hospitali.

“Kila maisha yana thamani na ni dhambi kubwa kukaa kimya, Waziri wa Afya ni muhimu kulichunguza hili na kulitolea tamko,” alisema mzazi huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Jackson.

 

WAZIRI WA AFYA

MTANZANIA lilimtafuta Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu taarifa hizo.

Waziri alisema tayari ameunda timu ya uchunguzi.

Alisema timu hiyo itatoka nje ya Muhimbili na itahusisha mtaalamu wa masuala ya oksijeni, muuguzi mwandamizi na daktari wa magonjwa ya watoto na   itatakiwa kukabidhi ripoti ndani ya siku saba.

“Taarifa nimeziona kwenye mitandao ya jamii… nimeunda timu ya uchunguzi ambayo itafanya kazi kwa siku saba kuchunguza ukweli wa tukio hili. Nikishapata taarifa hiyo nitatoa taarifa rasmi,” alisema Mwalimu.

 

UONGOZI MUHIMBILI

MTANZANIA lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha,  lakini alisema yuko likizo hivyo atafutwe msaidizi wake.

Alipotafutwa msaidizi wake, John Stephen, aliomba apewe muda afuatilie zaidi.

“Mimi sina taarifa, lakini naomba unipe muda nifuatilie zaidi nitakupigia,” alisema Stephen.

Baada ya muda ofisa huyo alimpigia mwandishi wa habari hizi na kusema kuwa watoto waliofariki dunia ni watatu.

“Kumbukumbu zetu zinaonyesha walifariki dunia watoto watatu tu, taarifa nyingine hazina ukweli wowote,” alisema Stephen.

Hata hivyo, ofisa huyo alisema leo itatolewa taarifa kamili kuhusu tukio hilo.

 

HALI HALISI VIFO VYA WATOTO

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria nchini kwa mwaka 2015- 2016 (TDHS- MIS) unaonyesha vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 51 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai hadi kufikia 43.

Licha ya matokeo hayo mazuri, bado kuna changamoto zinazochangia vifo vya uzazi kama vile ukosefu wa huduma za afya zenye kiwango kinachostahili na ukosefu wa vifaa tiba.

Lengo la tatu katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2015 – 2030) linasisitiza kuwa na maisha yenye afya na ustawi kwa wote, hivyo bado kunahitajika uwajibikaji wa pamoja kuboresha huduma za afya ya uzazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles