Serikali imesema haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini bali imechukua hatua ya kudhibiti matumizi ya fedha hizo ili kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji amesema hayo leo Jumatatu Januari 15, wakati akizungumza na wawakilishi wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya biashara nchini.
Dk. Kijaji amesema watu wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya nchi.
“Tatizo kubwa tunalokumbana nalo ni uhuru uliokuwapo awali ambao unasababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu kwani kila mmoja aliweza kutumia fedha za kigeni pia watumiaji wa fedha za kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti cha thamani ya kubadili fedha za kigeni,” amesema.
Amesema ili kuondoa changamoto hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu (BoT), ambayo inazitaka bei zote nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania.
“Bei hizi zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni, hata hivyo kama mlengwa akitaka kulipa kwa Shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni” amesema Dk. Kijaji.
Pamoja na mambo mengine, amesema mtu yeyote anayeishi nchini au nje ya nchi asilazimishwe kufanya malipo yoyote kwa kutumia fedha za kigeni kama ana Shilingi ya Tanzania mkononi mfano gharama za shule na hoteli.