NA AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amemfungulia kesi aliyemzushia kifo kupitia mitandao ya kijamii na amesema mtu huyo alikuwa na lengo la kumchafua na kuwavuruga wananchi ili wasifuatilie mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam baina ya Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa habari katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay alipofika kufungua kesi hiyo yenye RB namba OB/NB/613/2018 kwa lengo la kupata msaada wa Jeshi la Polisi ili kumbaini aliyetoa taarifa hizo za uongo Januari 9, mwaka huu ili amlipe fidia ya Sh bilioni 20.
“Lengo lilikuwa kuvuruga mkutano wa Magufuli na Lowassa, kwa hiyo wakajua labda ile habari ya Rais itasambaa sana atafanikiwa, wakaamua kuzusha kifo cha Mrema kwa sababu Mrema ni mtu mashuhuri, wakaona wakisema mimi hakuna mtu atawaza wala kuwafuatilia Lowassa na Magufuli,” alisema.
Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, alisema mbali na kuharibu mkutano huo pia habari za kifo chake zilimchafulia jina na kushindwa kufanya shughuli zake za kifamilia alizopanga kuzifanya kwa siku hiyo.
“Walitaka kuharibu kazi yangu niliyopaswa kuifanya Kilalaka, Marangu, siku hiyo nilitaka kwenda kujenga makaburi ya baba, mama na mdogo wangu aliyefariki, ni siku ambayo walikutana watu wengi kule pia nilitaka kusoma na misa ya kumshukuru Mungu kwa uzima alionipa lakini nikashindwa,” alisema.
Mrema alisema taarifa za kifo chake pia zilisababisha taharuki na vilio kwa wakazi wa kijijini kwake Marangu, familia yake na mtoto wake aliyepo nje ya nchi.
Kabla ya taarifa hiyo, alisema alipeleka malalamiko yake Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) waliompatia maelekezo ya kutoa taarifa polisi.
“Polisi wameniahidi wameanza kulifanyia kazi suala hili, nataka hii iwe fundisho kwa watu wote wanaozushia watu vifo maana kuna watu ambao hawana heshima na wenzao, huyu mtu akipatikana nataka anilipe fidia ya shilingi bilioni 20,” alisema.
Mrema alisema polisi wanapaswa wachukue hatua kali kwa wahusika kwa kuwa wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii vibaya na kusababisha hofu na majonzi kwa baadhi ya watu.