26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN: SMZ IMEJENGA UCHUMI KWA MIAKA MITATU

Na EVANS MAGEGE-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imefanya juhudi kubwa za kujenga uchumi ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya muhula wa pili wa uongozi wake.

Kauli hiyo aliitoa katika hotuba ya maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, marais wastaafu; Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na kupambwa kwa vijana wa halaiki, gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama na maandamano ya wananchi.

Wengine ni Rais mstaafu wa SMZ, Aman Abeid Karume, viongozi wengine waandamizi wa Serikali zote mbili na maelfu ya wananchi.

Katika hotuba yake aliyoisoma kwa takribani saa moja, Dk. Shein, alisema Serikali yake imechukua juhudi kubwa za kiuchumi kwa kuboresha ukusanyaji wa mapato.

Akifafanua juhudi hizo, alisema ndani ya mwaka jana pekee Serikali yake ilikusanya jumla ya Sh bilioni 548, kiwango ambacho ni cha juu zaidi ya mapato yaliyokusanywa mwaka juzi ambayo yalikuwa ni Sh bilioni 487.

“Mwaka jana mapato yameongezeka kwa shilingi bilioni 61, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.5 kwa kulinganisha na makusanyo ya kipindi kama hicho mwaka 2016,” alisema.

Dk. Shein alisema Pato la Taifa limeongezeka kutoka Sh bilioni 2,308 kwa mwaka 2015 na kufikia thamani ya Sh bilioni 2,628 kwa mwaka jana.

Pia alisema katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, utegemezi wa bajeti umefika kiasi cha asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 30 kwa mwaka 2010/2011.

“Kasi ya ukuaji wa uchumi inakuwa kwa kiasi cha asilimia saba kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016. Aidha, pato la mtu binafsi nalo limeongezeka kwa kufikia kiasi cha shilingi 1,800,006 ikilinganishwa na shilingi 1,632,000 kwa mwaka 2015,” alisema.

Kuhusu mfumuko wa bei, alisema kasi yake ulikuwa kwa asilimia 5.6 kwa mwaka jana kutoka asilimia 6.7 mwaka juzi.

Alisema lengo la Serikali yake ni kuimarisha uchumi na kuifanya Zanzibar kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.

Katika hatua nyingine, alisema katika kipindi cha Januari hadi Septemba, mwaka jana jumla ya miradi 25 ilipangwa na kuingiza mtaji wa kiasi cha Dola milioni 276 za Marekani.

Dk. Shein alisema miradi hiyo itakapokamilika inatarajiwa kutoa ajira 915.

Pia alisema kuanzia Julai, mwaka huu Serikali yake itaanza kutekeleza azma ya kurudisha utaratibu wa kutoa elimu bure katika shule za sekondari ili kutekeleza lengo la Mapinduzi.

“Kwa hivyo elimu ya msingi hadi ya sekondari itatolewa tena bure hapa Zanzibar kuanzia Julai, mwaka huu, hakutakuwa na mambo ya mzazi achangie elimu Zanzibar, sasa mzigo wote utabebwa na Serikali,” alisema.

Akizungumzia elimu ya juu, alisema kuna mafanikio makubwa na kwa sasa Zanzibar ina vyuo vitatu vinavyoendeshwa na wataalamu wa ndani.

Pia alisema sera ya afya ya mwaka 2014 imeelekeza kutolewa bure kwa huduma za afya hivyo kwa sasa huduma hizo zitatolewa katika hospitali 12 za Serikali badala ya tano zilizokuwapo kabla ya Mapinduzi.

Dk. Shein alisema huduma za afya bure pia zitatolewa katika vituo vya afya 158 badala ya 36 vilivyokuwapo kabla ya Mapinduzi.

Pia alisema kiwango cha madaktari kutoa huduma kimeimarika na wastani uliopo sasa daktari mmoja anahudumia watu 8,592.

Alisema kiwango hicho cha madaktari kuhudumia wagonjwa ni kizuri kwa kulinganisha na viwango vya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika hatua nyingine, katika kuelekea kilele cha Sherehe za Mapinduzi, jumla ya miradi ya maendeleo 33 ilizinduliwa na mingine 15 iliwekewa jiwe la msingi Unguja na Pemba.

Alisema uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi hiyo inahusisha miradi ya umeme, masoko, barabara, majengo ya Serikali, vituo vya afya, shule na kadhalika.

Alisema katika miaka mitatu ya kipindi cha pili cha uongozi wake, Serikali inaendelea vizuri kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kufuata dira ya maendeleo ya mwaka 2020 na lengo kuu ni kuhakikisha yanapatikana maendeleo yanayoridhisha.

Awali wakati akianza kusoma hotuba yake, Dk. Shein, alisema maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ni muhimu kwa Wazanzibari kwa sababu inawakumbusha walivyokata minyororo ya kikoloni na vibaraka wao.

Alisema uamuzi wa Mapinduzi ulitokana na wananchi wa Zanzibar kukataa madhila ya kutawaliwa waliyotendewa na utawala wa kisultani, wakoloni, mabwanyenye na mabepari waliowanyima wananchi haki zao za msingi katika kuendeleza maisha yao.

Alisema wananchi walibaguliwa kupewa huduma za afya, elimu, fursa za kuitumia ardhi yao, fursa za kazi zenye staha, heshima ya mwanadamu na kukosa makazi bora.

“Leo (jana) tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi ya miaka 54, hatuna budi kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu na waasisi wa Afro Shirazi walioongozwa na Rais wake wa kwanza marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kwa ushujaa wao wa kupigania haki zetu kwa kuleta usawa ndani yetu na kuondoa kila aina ya pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba.

“Leo (jana) ni siku ya ushindi wa Zanzibar na kwamba Mapinduzi yameweza kusimamisha utawala wa wanyonge, wakulima na kustawisha wafanyakazi, yaliweka usawa na kuwakabidhi tena wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar heshima na utu wao katika nchi yao,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles