32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NINI KINAENDELEA UPINZANI?

Na LEAH MWAINYEKULE


WAKATI wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, Tanzania kulikuwa kumechangamka sana.  Uchangamfu huu ulitokana na mambo mchanganyiko yaliyokuwa yakiendelea kipindi kiasi cha wengine kutoelewa mwelekeo hasa wa siasa za nchi ulikuwa upi.

 

Kwanza, ilianza kwa jina la Edward Lowassa kukatwa kati ya walioomba kugombea kiti cha Urais kwa kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Usiku ule ule wa jina lake kukatwa, wafuasi wake wengine walitamka wazi kupingana na jina la mgombea wao kutopitishwa.  Kesho yake hali iliendelea kuwa tete kwa wajumbe wa mkutano wa chama hicho nao kugawanyika, huku wengine wakiimba kwamba wana imani na mgombea aliyekatwa jina.

 

Haikuishia hapo. Katika siku zilizofuata, Lowassa alifanya uamuzi mgumu wa kukihama chama chake cha CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).  Awali wengine hatukutaka kuamini kwamba hilo linawezekana, lakini lilikuja kuthibitishwa na mwanachama huyo mpya ndiye aliyekuja kupitishwa kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chni ya muungano wa upinzani uliojulikana kama (Ukawa).

 

Lowassa si mtu pekee aliyeondoka CCM na kujiunga na upinzani.  Wapo wengine ambao walishindwa chaguzi za ndani ya chama chao – wengine wakitaka kugombea ubunge na wengine udiwani na waliamua kukimbilia upinzani wakidai kwamba chaguzi ndani ya CCM hazikuwa za haki na ziligubikwa na rushwa, hivyo mtu “mwadilifu” asingeweza kupitishwa kwa namna yoyote.

 

Ilikuwa ni kipindi cha uchaguzi, kwahiyo kutokana na hali yenyewe ya kisiasa ilivyokuwa imepata msisimko wa ghafla, wapiga kura waliamini kila kitu walichoambiwa na wale waliohamia upinzani.  Kipindi kile, wapiga kura walio wengi waliapa kwamba kura zao zitakwenda kwa wapinzani, hata kama huyo mpiga kura hajawahi hata kulisikia jina la mgombea kutoka chama cha upinzani, achilia mbali kuzijua sera zake na kile ambacho anapanga kukifanya kwa ajili ya kuleta maendeleo.

 

Na kweli, hamasa hiyo ilifanikisha wapiga kura wengi kupigia wagombea kutoka vyama vya upinzani, wakiwa na imani na wagombea wao kwamba huenda wakaleta mabadiliko na maendeleo ya kweli ambayo CCM inawezekana imeshindwa kuyaleta kwa kipindi kirefu.  Hata hivyo, miaka miwili tu baada ya watu hao kuchaguliwa kuwakilisha wananchi, wanaanza kujitoa mmoja baada ya mwingine na kuwaacha wapiga kura waliowaamini, kujiuliza ni lipi hasa linaloendelea.

 

Suala la wawakilishi wa wananchi kujivua uanachama wa vyama vyao na hivyo pia kuachia madaraka ya ubunge na udiwani, limetikisa katika wiki za hivi karibuni.  Kila wiki tunayoianza, watu wanajiuliza ni nani tena anayepanga kuita vyombo vya habari ama hata kujirekodi na kusambaza taarifa kwamba amekihama chama chake na kuamua ama kujiunga, au kurejea CCM.

 

Kinachoshangaza zaidi, ni sababu zinazotolewa za watu hao kujivua unachama na kuachia madaraka.  Wakati Lazaro Nyalandu ambaye alikuwa Mbunge wa Singida Kaskazini alipotangaza kujivua uanachama wa CCM pamoja na ubunge wake, alitoa sababu kwamba hafurahishwi na mambo ya siasa yanayoendelea nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, ongezeko la vitendo vya kidhalimu dhidi ya raia na kutokuwapo kwa mipaka baina ya mihimili ya Dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama.  Tulimwelewa na kuona sababu hizo kuwa za msingi.

 

Hata hivyo, hawa wengine wanaotoka upinzani na kujiunga na CCM, wanatoa sababu za kushangaza.  Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), kwa mfano, alidai amegundua kwamba Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani na imefanya kazi kubwa katika mambo mengi ambayo upinzani iliahidi kuyatekeleza.

 

Wiki chache zilizopita, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Siha, Dk. Godwin Mollel, naye alitangaza kujivua uanachama pamoja na wadhifa wake, kwa madai kwamba ameona nia ya dhati ya Serikali ya CCM kutetea rasilimali za Taifa.

 

Mtu pekee ninayeweza kumuelewa kuihama Chadema ni Lawrence Masha, ambaye baada ya kushindwa kwenye kura za maoni ya kugombea kiti cha ubunge kupitia CCM alikimbilia Chadema kuungana na Edward Lowassa aliyekuwa amejiunga huko wakati huo.  Kwa kifupi, Masha alikuwa anatanga tanga na kutokuwa na msimamo na sasa amerejea ambako ndiko moyo wake ulipo.

 

Lakini wakati huo huo, aliyenisikitisha zaidi ni David Kafulila, ambaye hata yeye mwenyewe alilalama sana kwamba CCM ilinyang’anya ushindi wake wa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita katika Jimbo la Kigoma Kusini.  Tena mtu huyu alilalama kwa machozi na kusababisha aonewe huruma na karibu kila mtu.  Leo hii anajivua uanachama wa Chadema na kujiunga huko huko CCM alikolalama aliibiwa ushindi wake, huku akidai kwamba haoni upinzani kuwa na nia ya dhati ya kupambana na ufisadi.

 

Jamani, nchi hii tunahitaji kuwa na upinzani wenye nguvu.  Kama nchi tulikubali kuingia katika siasa za vyama vingi kwa ajili ya kukuza demokrasia na ni wazi kwamba japo bado zipo changamoto, uwepo wa vyama vya upinzani, kuhoji kwa vyama vya upinzani, usumbufu wa vyama vya upinzani, vimefanikisha Serikali kujitathimini mara mbili mbili katika uamuzi wake.

 

Suala la Serikali ya CCM kusimamia Ilani yake, ni kazi yake halali kabisa na ndicho kinachotakiwa.  Kusema kwamba eti unajiondoa upinzani na kujiunga na CCM kwa kuwa Serikali inasimamia Ilani yake, ni kuwafanya wapiga kura waliokuchagua kama hawakuwa na kazi ya kufanya.  Walikuchagua ili uibane Serikali na kufanikisha itekeleze ilani yake na kuleta maendeleo kwa nchi,  tatizo liko wapi hapo?

Kama Serikali inafanya kazi nzuri, inaleta maendeleo, inapambana na ufisadi, inatekeleza ilani yake, inatekeleza hata mengine yaliyoahidiwa na upinzani, hiyo si ndio sababu tosha ya upinzani kujisifia kwamba inafanya kazi nzuri ya kuibana Serikali kiasi cha Serikali hiyo kulazimika kutekeleza yale yaliyo ya maendeleo ili isipakwe matope?

 

Cha zaidi, wapiga kura wanapochagua mwakilishi kwa ajili ya kuwawakilisha iwe bungeni ama kwenye Baraza la Madiwani, vina uhusiano gani na Serikali kutekeleza ilani yake?  Yaani wapiga kura wanalazimika kufanya uchaguzi mwingine utakaotumia muda pamoja na mamilioni ya fedha kwa sababu tu ya mihemko ya mtu ambaye hakuwa na uhakika na mustakabali wake wa kisiasa?

 

Sitaki kuamini kwamba sababu zinazotolewa na watu wanaojivua uanachama, kuwa za kweli.  Nataka kuamini kwamba wameamua kuzitoa sababu hizo kwakuwa hawakutaka kusema ukweli, lakini ipo sababu nyingine nyuma ya pazia inayosababisha haya yanayotokea, yawepo.  Ni nini hasa kinachoendelea huko upinzani?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles